TAARIFA zinasema kwamba, Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ amefuatwa nyumbani kwao Burundi na viongozi wa timu moja kutoka Uarabuni kwa ajili ya mazungumzo ili kumsajili.
Saido ambaye hivi karibuni aliondoka Tanzania kwenda Burundi kwa ajili ya mapumziko mafupi, wakati akiwa huko ndipo Waarabu hao walipomuibukia kwa nia ya kumshawishi wamsajili.
Nyota huyo aliyetua Yanga dirisha dogo la msimu uliopita, mkataba wake unatarajiwa kumalizika
mwisho wa msimu huu.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Hivi karibuni Saido akiwa kwao Burundi alifanya kikao na mwakilishi wa timu kutoka Uarabuni ambayo siwezi kuitaja.
“Anaweza kukubali dili hilo maana lina pesa nyingi, ila kwa upande wa viongozi wa Yanga wamemwambia asubiri wakimaliza Mapinduzi wataongea naye kujadili mkataba mpya.”
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema: “Kuhusu suala la Saido lazima ataongezewa mkataba.”
Kwa sasa Yanga inajiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC ambao ni wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na Yanga ni mabingwa watetezi.