>

ISHU YA KIPA MPYA YANGA MENGINE YAIBUKA

WAKATI Yanga ikitajwa kwamba imemalizana na kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Aboutwalib Msheri kujiunga na Yanga, mabosi wa Mtibwa Sugar wameweka wazi kuwa badO mchezaj huyo ni mali yao na hawajamuuza.

Hapo awali, Yanga ilizungumza na Msheri na Mtibwa kuhusu kumvuta mitaa ya Jangwani lakini Mtibwa waliweka ngumu wakidai kuwa bado wanamuhitaji kipa huyo hivyo hauzwi kwa gharama yeyote ile.

Mtibwa walidai kuwa kwa sasa timu yao ipo kwenye kipindi cha mpito kwenye ligi hivyo haiwezi kumuachia Msheri kwani ni moja kati ya wachezaji tegemeo ndani ya kikosi hicho ambacho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kipo nafasi ya 13 na pointi 10.

Jambo hilo liliwaumiza kichwa Yanga na kutaka kufanya uamuzi mgumu wa kwenda nje ya nchi kutafuta kipa mkali lakini wakasikilizia kuona kama Mtibwa watatulia.

Taarifa kutoka ndani ya Mtibwa zinaelezwa kuwa baada ya yote hayo, Msheri aliwaambia mabosi wake kuwa hawezi kucheza tena kwa furaha kwani mawazo na akili yake tayari ameihamishia kwenye dili la Yanga na kuomba auzwe tu lakini mabosi hao wakagoma pia.

Baada ya hapo Msheri na baadhi ya watu wake wa karibu waliandika barua ya kuomba kuvunja mkataba na hapo ndipo Mtibwa wakawaita Yanga mezani tena.

Msheri alisaini mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa msimu huu na Mtibwa ambao utamalizika mwishoni mwa msimu ujao lakini hadi sasa alikuwa ameutumikia kwa nusu msimu.

Katika vipengele hivyo inaelezwa kuwa kuvunja mkataba huo kulihitaji Shilingi za Kitanzania milioni 20, pesa ambayo Msheri yupo tayari kuilipa ili ajiunge na Yanga lakini Mtibwa ni kama wamebadili gia na kutaka mazungumzo upya na Yanga.

“Niseme tu Abou Twaleeb mshery ana mkataba na Mtibwa Sugar, huyu tumemlea kwa miaka 6 na huu ni msimu wake wa 2 kuaminiwa katika kikosi cha kwanza cha Mtibwa.

“Yeye ni pacha wa Kibwana Shomary, Yeye ni pacha wa Dickson Job, hawa wote walikuja pamoja. Kuhusu kwenda Yanga sisi wenyewe tunasikia kwenye mitandao, kama wanamuhitaji waje mezani sisi tupo tayari kuzungumza nao”

Sisi kama chuo cha mpira Tanzania, vijana wengi wanatamani kurithi nafasi yake kwahiyo tupo tayari kumuachia kama tutafikia makubaliano kwenye mazungumzo yetu,” amesema Thobias Kifaru, Afisa Habari Mtibwa Sugar.