>

KIUNGO MPYA YANGA KUKUNJA MILIONI 158

IMEFAHAMIKA kuwa Yanga imetumia kitita cha Sh 50Mil kwa ajili ya kununua mkataba wa kiungo mshambuliaji wa Biashara United, Denis Nkane huku ikimpa mshahara wa Sh mil 3 kwa mwezi.

Nkane ni kati ya wachezaji waliokuwa wanawaniwa vikali na timu kongwe za Yanga na Simba ambayo ilizidiwa ujanja katika kuwania saini ya kiungo huyo kinda.

Yanga tayari imemtambulisha kiungo mchezeshaji fundi, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ baada ya kuvunja mkataba na Azam FC.

Ndani ya miaka mitatu kwa mshahara wa mil 3 kwa mwezi, Nkane jumla ataingiza Sh mil 108 na ukijumlisha na dau lake la usajili Sh 50M, itakuwa Sh mil 158.

Taarifa kutoka kwa chanzo cha habari kutoka Yanga, kiungo huyo tayari amesaini mkataba mrefu wa miaka mitatu katika dirisha dogo kwa ajili ya kuichezea Yanga.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, kiungo huyo muda wowote atatambulishwa na uongozi wa Yanga akiwa amevalia jezi zenye rangi ya kijani na njano kama ilivyokuwa kwa Sure Boy katika mitandao yao ya kijamii.

Aliongeza kuwa kwa dau hilo la usajili, kiungo huyo amesaini mkataba wa miaka mitatu ya kwenda kuichezea Yanga ambayo hivi sasa inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 26.

“Haikuwa rahisi kufanikisha usajili wa Nkane kutokana na kuwepo katika mipango ya kusajiliwa na baadhi ya timu kubwa hapa nchini.

“Hadi tunampata nguvu kubwa tuliitumia viongozi, kwa kumpatia dau la fedha la Sh 50Mil katika misimu mitatu atakayocheza Yanga.

“Pia kiungo huyo tofauti na dau hilo, pia atapatiwa nyumba ya kuishi nje ya kambi, huo umekuwa utaratibu wetu tukiufanya kwa wachezaji kutoka nje ya nchi na mikoani,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said juzi alisema kuwa: “Tumepanga kufanya usajili mkubwa utakaoendana na mapendekezo ya usajili ya kocha kutoka katika ripoti yake aliyoikabidhi kwa uongozi.”

Chanzo:Championi