HIVI NDIVYO SIMBA WALIVYOTOA ZAWADI YA KRISMASI

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba jana Desemba 24 wametoa zawadi ya Krismasi kwa mashabiki wake baada ya kusepa na pointi tatu mazima mbele ya KMC.

Baada ya dakika 90 kukamilika ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulisoma KMC 1-4 Simba ikiwa ni ushindi wao wa kwanza kushinda mabao zaidi ya matatu kwenye mchezo mmoja na wa pili kushinda mabao mengi ilikuwa mbele ya Ruvu Shooting ubao wa Uwanja wa CCM Kirumba uliposoma Ruvu Shooting 1-3 Simba.

Mabao ya Simba yalipachikwa na Mohamed Hussein dakika ya 10 kwa pasi ya Jonas Mkude ambaye alipiga faulo akiwa nje ya 18 na dakika mbili mbele Simba ilipachika bao la pili kupitia kwa Joash Onyango ambaye aliunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Rally Bwalya.

KMC hawakuwa nyuma waliweza kufanya shambulizi kali dakika ya 41 ambapo kwa kupitia pasi ndefu ya Emmanuel Mvuyekule dakika ya iliweza kumfikia Abdul Hillay aliyemtungua Aishi Manula.

Dakika 45 za awali zilikamilika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao hayo mawili huku KMC wakiwa wamepata bao moja.

Kipindi cha pili Simba walianza kwa kasi ambapo dakika ya 46 walipachika bao la tatu kupitia kwa Kibu Dennis ambaye alitumia makosa ya safu ya ulinzi ya  KMC kisha alipachika bao la nne dakika ya 46 akimalizia pasi ya Shomari Kapombe.

Hivyo kipa namba moja wa KM, Faroukh Shikao nyavu zake zilitikiswa mara nne huku wa Simba, Aishi Manula akitunguliwa mara moja.

KMC walikosa umakini ambapo ilibaki kidogo wapachike bao la pili kupitia kwa Matheo Anthon ilikuwa dakika ya 71 lakini shuti lake lilikwenda nje ya lango.

Simba inafikisha pointi 21 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 9 na vinara ni Yanga wenye pointi 23 nao pia wamecheza mechi 9.