NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kwamba hakuna mchezaji mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa kuwa Yanga ni kubwa kuliko yoyote.
Kocha huyo raia wa Tunissia ameongeza kuwa kuhusu kuanza kikosi cha kwanza kwa wachezaji wake itategemea na namna hali itakavyokuwa kutokana na mchezo husika na haina maana kwamba kufunga mabao ni sababu ya kuweza kuanza kikosi cha kwanza.
Ikumbukwe kwamba nyota wake Heritier Makambo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ihefu FC uliochezwa Uwanja wa Mkapa aliweza kufunga mabao matatu lakini Nabi amebainisha kwamba hawezi kuwa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza.
“Kila mchezaji ndani ya Yanga ni muhimu na ipo wazi kwamba Yanga ni kubwa kuliko mchezaji hivyo haina maana kwamba kufunga ama kutofunga ni sababu za mchezaji kuanza kikosi cha kwanza.
“Ninafurahishwa na uwezo wa wachezaji wangu wote kila mmoja anatimiza majukumu yake kuhusu kuanza ama kutokuanza kikosi cha kwanza wote wanastahili kucheza na inategemea na mbinu ya mchezo husika,”amesema.