KOCHA YANGA AKOSOA MFUMO WA KOCHA MPYA SIMBA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amekosoa mfumo wa kocha mpya wa Simba, Pablo Franco kuwa ni wa tofauti na ule uliokuwa ukitumika na kocha aliyepita Didier Gomes.

Nabi amesema kuwa kuna tofauti kubwa ya uchezaji ambao upo ndani ya Simba kwa wakati huu baada ya kupata kocha mpya ambaye ni Franco.

“Kuna mabadiliko kwenye upande wa uchezaji unaona kwamba kwa sasa kocha huyu (Franco) anapenda kujilinda tofauti na aliyepita, (Gomes) ambaye alikuwa anapenda kushambulia muda mwingi,” alisema Nabi.

Gomes aliomba kuondoka ndani ya Simba Oktoba 26 baada ya timu hiyo kutokewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy, Uwanja wa Mkapa.

Kwa sasa mikoba yake ipo mikononi mwa Franco ambaye alikiongoza kikosi hicho kwa mara ya kwanza kwenye Kariakoo Dabi mbele ya Yanga na kutoshana nguvu bila kufungana.