KOCHA AZAM FC ATAJWA KUFUTWA KAZI

UONGOZI wa klabu ya Azam FC umesitisha mkataba wa Kocha kutoka nchini Zambia George Lwandamina na Msaidizi wake kutoka Burundi Vivier Bahati, kutokana na mwenendo mbaya wa kikosi chao kwenye Mshime Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

Azam FC jana Jumapili (Desemba 12) ikicheza nyumbani Azam Complex Chamazi, iliambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar, hivyo imefikisha michezo miwili iliotoka sare, kushinda mitatu na kupoteza mitatu, huku ikishika nafasi ya 7 kwenye msimamo.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ya Dar es salaam zinaeleza kuwa, kocha Abdihamid Moallin raia wa Marekani atakaimu nafasi ya George Lwandamina, hadi Kocha mpya atakapotangaza.

Moallin ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa D.C United ya MLS na Horseed ya Somalia aliajiriwa na Azam FC mwezi Novemba kama Mkurugenzi wa Ufundi wa kituo cha kukuza na kuelea vipaji. Raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Somalia licha ya kuwa kocha pia ana ujuzi wa kuchambua soka ‘Match Analysis’.

Alipotafutwa kocha huyo ambaye anatajwa kupewa mikoba ya Lwandamina aliweka wazi kwamba hana taarifa zozote.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC,Abdulkarim Amin alipotumiwa ujumbe kuhusu kufutwa kazi kwa Lwandamina hakuweza kujibu.

Ofisa Habari wa Azam FC,Zakaria Thabit alipotafutwa kupita simu yake ya mkononi hakuweza kupokea.