SIMBA KIMATAIFA INA KAZI KUBWA

    WAMESHINDA katika hilo nakubali walicheza mchezo wao kwa kujituma na nyota wao akiwa ni Bernard Morrison hapo kuna jambo linapaswa kufanyiwa kazi.

    Kwa wale wanaopenda mpira wanajua maana ya kucheza kama timu na kucheza kwa mchezaji mmoja hapo kwa wawakilishi wetu Simba kimataifa lazima washtuke.

    Mchezo wao ujao dhidi ya Red Arrows sio wa kitoto na wanapaswa wakumbuke kwamba watakuwa ugenini sasa hapo hakuna anayejua kwamba itakuaje kwa mara nyingine ugenini.

    Ukweli ni kwamba mashindano ya kimatafa ni tofauti sana na ligi ya ndani kwa namna yoyote, popote kokote unapokuwa unaweza kufungwa na kufunga pia.

    Basi kwa kuwa mchezo wa kwanza Simba ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Red Arrows, Uwanja wa Mkapa basi kituo chao kinachofuata ugenini ni lazima wafanye kweli kwa kucheza wakiwa ni timu na wasitegemee mchezaji mmoja.

    Kwa namna ambavyo Kocha Mkuu, Pablo Franco ameanza kazi yake kwa kupata ushindi basi anapaswa kuwa bega kwa bega na wachezaji pamoja na viongozi wengine  ili kuweza kupata matokeo chanya kwenye mechi zijazo.

    Hapo kazi ijayo ikiwa wachezaji watajisahau na kwenda na ile hali ya kujiamini tutarajie anguko kubwa na lile la kutisha kuliko la Jwaneng Galaxy kwa kuwa wale wapinzani wa Simba sio wa kubeza.

    Tatizo kubwa ambalo linapaswa kufanyiwa maboresho ndani ya Simba ni kufanyiwa maboresho kwenye upande wa washambuliaji pamoja na wapigaji mapigo huru.

    Unajua kwa wakati huu soka ambalo linabadilika inapaswa kila mchezaji kuwa makini katika adhabu ambazo wanapata hasa mapigo huru.

    Kwa sasa imekuwa kama hakuna mpigaji wa penalti pamoja na mpigaji wa faulo kwa kuwa mipira mingi ambayo wanapata yanakwenda na maji.

    Ni Bwalya pekee ambaye aliweza kufunga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Polisi Tanzania huku Bernard Morrison akikosa mbele ya Red Arrows kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho.

    Wapinzani wao Red Arrows wanaonekana kuwa bora katika eneo hilo hivyo ili iweze kuwa vizuri kwa wakati ujao ni lazima Simba wajipange katika eneo hili wawe bora zaidi.

    Pia kwenye upande wa mabeki ni lazima waongeze umakini mara dufu katika kulinda lango lao kwa kuwa makosa yao yamekuwa ni ya kujirudia hasa kwa kukaba kwa macho ilihali wanahitaji kupata ushindi.

    Kila la kheri Simba na mnastahili pongezi kwa namna ambavyo mnafanya kazi kubwa uwanjani kusaka ushindi mnawakilisha Tanzania na taifa kiujumla.

    Iwe katika wakati bora kwa ajili ya Tanzania na dunia kiujumla basi pambaneni kwa juhudi bila kukata tama na inawezekana kufanya vizuri na kusonga mbele katika hatua ya makundi.

    Kutanguliza mguu mmoja haina maana mmekamilisha kazi huo mguu mwingine ambao umebaki basi hakikisheni kwamba unakwenda mbele na mnapata kile ambacho mnastahili.

    Hatua moja kila wakati hakuna haja ya kukata tamaa sijui itakuaje ikiwa mtapoteza ugenini wakati mna mtaji wa mabao mliyofunga? Msifikiri kazi imekwisha ukurasa ndo kwanza unafunguliwa.

    Previous articleISHU YA USAJILI AZAM FC IPO HIVI
    Next articleMKATABA WA GSM NA TFF UNACHUNGUZWA