>

MKATABA WA GSM NA TFF UNACHUNGUZWA

TUME ya Ushindani wa Biashara (FCC) imesema imepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa mpira wakiitaka kuchunguza udhamini uliofanywa na kampuni ya GSM kwa Ligi Kuu ya NBC kama hautaathiri ushindani wa soka nchini.

 

Wadau hao wamewasilisha malalamiko yao kwa maandishi ndani ya tume hiyo Jumatatu ya Novemba 29, 2021 wiki hii kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa FCC, William Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari.

 

Aliyasema hayo alipokuwa akitangaza maadhimisho ya siku ya ushindani duniani yanayotarajiwa kufanyika Desemba 6 mwaka huu kwa upande wa Tanzania. Mtendaji huyo alisema kama tume itakuja na tamko maalumu juu ya suala hilo baada ya kujiridhisha.

 

Malalamiko hayo yamepokelewa ikiwa ni siku chache tangu kampuni ya GSM kusaini mkataba wa Sh2.1 bilioni na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF). Mkataba huo uliosainiwa Novemba 23, 2021 unaifanya kampuni hiyo kuwa mdamini mwenza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania inayoshika nafasi ya nane kwa ubora Afrika ambayo kwa sasa inadhaminiwa na NBC.

 

Hilo limefanayika ikiwa ni muda mchache tangu kampuni hiyo ambayo ni mdhamini wa Yanga SC kutangaza kuzidhamini timu za Pamba na Coastal Union ya jijini Tanga.

 

“Tulishaanza mchakato wakutaka kujua kama kitendo hicho hakitaathiri ushindani katika soka na majibu ya suala hili yatatolewa baada ya kujiridhisha kwa kuzingatia kanuni za ushindani na kama kweli linahusiana na ushindani,” alisema Erio.

 

Alisema katika barua waliyopokea miongoni mwa vitu vilivyohojiwa ni Je kwa kufanya hivi hakutaathiri ushindani na Yanga haitanufaika zaidi katika mashindano hayo kwa sababu mdhamini wao amedhamini na timu nyingine pia.

 

“Hilo siwezi kulisemea kwa sasa kwa sababu tunalifanyia kazi. Sisi ni kama Mahakama mtu anaweza kufungua kesi ambayo hata haina msingi lakini huwezi kumuambia haina msingi kabla ya kuipitia hivyo itapangiwa Hakimu au Jaji itasikilizwa baadaye inatupiliwa mbali au kutolewa maamuzi.

 

“Sasa kufanikisha hili tunaomba taarifa fulani kutoka vyombo mbalimbali na tutaangalia kama itaathiri kwa namna yoyote ile katika ushindani,” alisema Erio.