>

NAMNA SIMBA WALIVYOICHAPA 3-0 RED ARROWS KWA MKAPA

KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco jana Novemba 28  kilitupa kete ya kwanza kwenye mchezo wa mtoano katika Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa mabao 3-0.

Kasi ya Simba ilianza katika dakika 45 za mwanzo ambapo ni Bernard Morrison raia wa Ghana alifunga bao la kwanza kwa pigo huru ilikuwa dakika ya 16 akiwa nje ya 18 kwa faulo ambayo alichezewa yeye mwenyewe.

Baada ya dakika mbili Simba waliweza kupachika bao la pili ambapo ilikuwa dakika ya 19 baada ya Morrison mzee wa kuchetua kusepa na kijiji cha wachezaji wawili akiwa ndani ya 18 na kutoa pasi kwa Meddie Kagere ambaye aliujaza moja kwa moja kwenye nyavu.

Bado Simba walizidi kuliandama lango la Red Arrows ambapo dakika ya 29, Hassan Dilunga alichezewa faulo ndani ya 18 na mwamuzi akaamua ipigwe penalti kuelekea lango la Arrows.

Haikuwa bahati kwa mpigaji Morrison mpira wake uliokolewa na kipa wa Red Arrows na kufanya Simba wakose penalti kwenye mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa na walikwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 2-0 Red Arrows.

Kipindi cha pili, Arrows walirejea kwa kasi kusaka bao la kusawazisha kwa Simba ila uimara wa mikono ya Aishi Manula uliweza kuokoa michomo ya hatari iliyokuwa inapigwa na wapinzani hao.

Bao la tatu lilipachikwa na Morrison kwa shuti lililompita kwenye miguu kipa wa Red Arrows, ilikuwa ni dakika ya 77 na kuwafanya wawarudishe tena wapinzani wao kwenye eneo la kati.

Unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu, Pablo Franco kuweza kukaa benchi na kushuhudia ushindi huo kwenye mchezo wa kimataifa.

Red Arrows sio watu wazuri kwa kuwa walicheza zaidi ya faulo 16 ndani ya dakika 90 jambo ambalo linaonyesha kwamba sio timu ya kuibeza kuelekea kwenye mchezo wa marudio ambapo Simba itakuwa ugenini katika mchezo wa pili.

Nyota wa mchezo alikuwa ni Morrison licha ya Uwanja wa Mkapa kuwa na maji mengi baada ya mvua kunyesha bado aliweza kuhusika kwenye mabao yote matatu ambapo alifunga mabao mawili na pasi moja katika mchezo huo.