KAZI imeanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco baada ya kushuhudia namna Ligi Kuu Bara inavyokwenda na kasi ya wachezaji wake ambao alianza nao kikosi cha kwanza.
Baada ya kuchukua mikoba ya Didier Gomes kete yake ya kwanza ilikuwa mbele ya Ruvu Shooting, Uwanja wa CCM Kirumba na ubao ulisoma Ruvu Shooting 1-3 Simba.Haya hapa mambo ambayo aliyashuhudia akiwa kwenye benchi kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya ushindani:-
Manula
Aishi Manula kwenye mechi zake tano ambazo alikuwa ameanza alikuwa shujaa kwa kuwa hakuruhusu bao ila mbele ya Pablo alishindwa kuendeleza ubabe wake na kuokota bao kwenye nyavu zake ilikuwa dakika ya 70 na mtupiaji alikuwa ni Elias Maguli.
Shomari Kapombe
Jukumu lake kubwa ni kumwaga majalo akitokea pembeni na alitimiza majukumu yake kwa kuwa bao la kwanza, kona alisababisha dakika 17 ikapigwa na Bernard Morrison na kukutana na Meddie Kagere ambaye alitupia bao la kuongoza na lile la tatu dakika ya 44 lililofungwa na Kibu Deniss mguso ulianzia kwake na ukapigwa kisigono na Kagere aliyetoa pasi ya bao kwa Kibu.
Mohamed Hussein
Alikuwa na kazi kubwa kuendeleza kuonyesha makeke yake na alikuwa na jukumu pia la kupiga mipira iliyokufa ambapo alipiga faulo moja .
Joash Onyango
Mzee wa kutibua mipango, Rashid Juma winga wa Ruvu Shooting na Shaban Msala hawa walikuwa wakikutana na kisiki cha Onyango ambaye mipira yake yote mirefu ilikuwa ikishindwa kuwafikia walengwa.
Pascal Wawa
Kwenye ubora wake licha ya kushuhudia bao moja wakifungwa kutokana na uzembe aliweza kupiga shuti moja ambalo liliokolewa na kipa Mohamed Makaka.
Jonas Mkude
Kiungo ambaye amerejea kwa kasi na kuonyesha ubora wake eneo la kati na alikuwa akirudi nyuma kuweza kulinda lango la Manula.Ngoma ilikuwa nzito kupenya hasa kipindi cha pili ambapo Ruvu Shooting waliwasha taa zote nyekundu.
Hassan Dilunga
Moja ya viungo ambao ni wasumbufu uwanjani muda wote alikuwa akipambana kusaka ushindi na alipiga shuti moja ambalo halikulenga lango ilikuwa dakika 26.
Mzamiru Yassin
Kiungo punda, kiungo wa kazi chafu alikuwa ni mzee wa kucheza faulo ambapo aliweza kugongana mara mbili na nyota wa Ruvu Shooting, alikwama kukamilisha dakika 90 kwa kuwa aliumia dakika ya 68 na nafasi yake ilichukuliwa na Erasto Nyoni.
Meddie Kagere
Alihitaji dakika 68 kufunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao na kuwa nyota wa mchezo kwa upande wa Simba.
Kibu Dennis
Bado amekosa utulivu licha ya kufunga bao moja dakika ya 44 alikosa nafasi ya wazi dakika ya 90 na aliweza kusababisha penalti dakika ya 71 iliokolewa na Mohamed Makaka baada ya Nyoni kuipiga.
Morison Bernard
Mzee wa kuchetua hakuwa na bahati licha ya kutoa pasi moja ya bao na kupewa jukumu la kupiga mipira yote iliyokufa ambapo alipiga jumla ya kona 8 alionyeshwa kadi ya njano mapema dakika ya tano.
Akiongeza umakini anaweza kuwa bora kwa kuwa alikosa nafasi ya wazi dakika ya 60.
Pablo aliweza kuishuhudia Ruvu Shooting, ‘Barcelona ya Bongo’ ikiwa imara kupitia kipa wao namba moja Mohamed Makaka ambaye mbali na kuokoa penalti dakika ya 71 iliyopigwa na Erasto Nyoni alikokoa michomo minne kipindi cha kwanza na kipindi cha pili ilikuwa ni mitatu.
Rashid Juma,Shaban Msala hawa walimpa tabu Pablo na hata nahodha wa Ruvu Shooting, Fully Zullu Manganga alikuwa mchezaji wa kwanza kufanya jaribio lililookolewa na Manula ambaye alionja joto ya jiwe kupitia bao la Elias Maguli.