Home Sports TANZANIA YASHUKA VIWANGO FIFA

TANZANIA YASHUKA VIWANGO FIFA

TANZANIA imeshuka nafasi moja kutoka 130 hadi 131 katika viwango vya ubora wa soka vilivyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, Fifa jana.

 

Huenda kufanya kwao vibaya katika michezo miwili ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) waliofungwa mabao 3-0 na sare ya bao 1-1 dhidi ya Madagascar kumeiporomosha.

 

Tanzania ilishindwa kufuzu na kuishia hatua ya makundi katika Kundi J, ikimaliza kwa kushika nafasi ya tatu kwa pointi nane, huku kinara DRC ikisonga mbele hatua ya mtoano kwa pointi 11. Nafasi ya pili ilishikiliwa na Benin iliyokuwa na pointi 10 na Madagscar ilikuwa ya mwisho kwa pointi nne.

 

Aidha, kwa upande wa Afrika Mashariki Uganda bado wanaongoza wakishika nafasi ya 82, wakifuatiwa na Kenya 102, Sudan 124, Ethiopia 135 na Burundi 140. Kwa upande wa Afrika Senegal, Morocco, Tunisia, Algeria, Nigeria, Misri na Cameroon zipo katika 50 bora.

 

Kidunia, Ubelgiji ndio inaongoza ikifuatiwa na Brazil, Ufaransa, England, Argentina, Italia, Ureno, Denmark na Uholanzi.

Previous articleKIKOSI CHA YANGA KINACHOTARAJIWA KUANZA LEO DHIDI YA NAMUNGO
Next articleRASMI,KIKOSI CHA YANGA DHIDI YA NAMUNGO