MWENDO ALIOANZA NAO PABLO BONGO HUU HAPA

PABLO Franco Kocha Mkuu wa Simba ameanza kwa kushuhudia timu yake ikisepa na ushindi mbele ya Ruvu Shooting kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Ukiwa ni mchezo wake wa kwanza baada ya kuchukua mikoba ya Didier Gomes alishuhudia  ubao ukisoma Ruvu Shooting 1-3 Simba ambapo mbinu yake ya kuwatumia washambuliaji wawili Kibu Dennis na Meddie Kagere ilijibu kipindi cha kwanza.

Watupiaji walikuwa ni Meddie Kagere ambaye alitupia mabao mawili ilikuwa dakika ya 17 na 36 huku lile la tatu likifungwa na Kibu Dennis dakika ya 44.

Linakuwa ni bao la kwanza kwanza kwa Kibu ndani ya Simba akitumia pasi ya Kagere ambaye alikuwa ni nyota wa mchezo jana kwa kuwa alihusika kwenye mabao yote matatu.

Ruvu Shooting ilikuwa imara upande wa kipa ambapo Mohamed Makaka aliweza kuokoa michomo sita kwenye mchezo huo ikiwa ni pamoja na penalti iliyopigwa na Erasto Nyoni dakika ya 71 iliyosababishwa na Kibu aliyechezewa faulo na Zuberi Dabi.

Kiungo Bernard Morrison anaingia kwenye rekodi ya mchezaji wa Simba ambaye ameonyeshwa kadi ya njano mapema ilikuwa ni dakika ya tano baada ya kuonekana akijibizana na mwamuzi kwa kile alichokuwa anahitaji apewe penalti kwa kuwa alichezewa faulo ndani ya 18.

Pia Morrison alipewa jukumu la kupiga kona ambazo zilipatikana kwenye mchezo huo na kipindi cha kwanza pekee alipiga kona nne na moja ilisababisha bao lililofungwa na Kagere dakika ya 36.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 14 ikiwa nafasi ya pili huku ile ya kwanza ipo mikononi mwa Yanga yenye pointi 15.

Elias Maguri ni yeye ambaye alitibua rekodi ya clean sheet ya Aishi Manula kwa kupachika bao dakika ya 70 ni yeye pia alitibua rekodi ya clean sheet za Manula ambaye alikuwa amekaa langoni kwenye mechi tano bila kufungwa.