>

NAMUNGO V YANGA, YUPI ATAVUNJA NGOME LEO?

 

ILE ngome ambayo ilikuwa ngumu kuvunjika muda wote sasa wakati wake umefika tena kuanza kuvunjwa upya ambapo leo Uwanja wa Ilulu, wanaume watakuwa kazini.

Baada ya kushindwa kufanikiwa kwa muda wa misimu miwili walipokutana wanakutana kwa mara nyingine tena kuendelea pale walipoishia ili kuweza kuona baada ya dakika 90 kitatokea kitu gani.

Utakuwa ni mchezo wa ligi kati ya Namungo iliyo nafasi ya 12 na pointi tano dhidi ya vinara wa ligi, Yanga wakiwa na pointi 15, mwendo wao ulikuwa namna hii:-

Dakika 360 hakuna mbabe

Timu hizi ndani ya dakika 360 kwenye mechi nne ambazo walikutana uwanjani hakuna mbabe ambaye aliweza kusepa na pointi tatu mazima zaidi ilikuwa ni mwendo wa kugawana pointi mojamoja.

Machi 15, Uwanja wa Majaliwa, msimu wa kwanza kwa Namungo kupanda Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Mkuu, Hitimana Thiery ambaye kwa sasa yupo ndani ya Simba akiwa ni kocha msaidizi ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kucheza na Namungo Uwanja wa Majaliwa.

Dakika 90 ngoma ilikuwa nzito na timu zote zilifungana bao mojamoja na waligawana pointi mojamoja.

Walipokutana Dar, Uwanja wa Mkapa, ubao ulisoma Yanga 2-2 na kuwafanya wagawane tena pointi mojamoja hivyo kwa msimu wa kwanza ngoma ilikuwa ngumu nje ndani.

2020/21 mwendo uleule

Msimu wa 2020/21 mchezo wa kwanza Uwanja wa Mkapa wakati huo Kocha Mkuu alikuwa Cedric Kaze kwa Yanga sasa ni kocha msaidizi ubao ulisoma Yanga 1-1 Namungo.

Mchezo wa pili ilikuwa Uwanja wa Majaliwa ilikuwa ngumu kwa timu zote kushinda ubao ulisoma Namungo 0-0 Yanga wakagawana tena pointi mojamoja.

Siku nyingine mahali pengine

Leo ni siku nyingine na wakati mwingine wababe hawa wanakutana. Haitakuwa Uwanja wa Majaliwa bali ni Uwanja wa Ilulu hapo rekodi mpya inasubiriwa kuona nani atakuwa nani ama mwendo utabaki uleule wa sare ni jambo la kusubiri.

Watakaokosekana

David Molinga mshambuliaji wa Namungo atakosekana kwenye mchezo kwa kuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu pamoja na Kocha Mkuu wa Namungo Hemed Morroco naye anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatupamoja na Makame.

Kwa upande wa Yanga ni Mapinduzi Balama,Dickson Ambundo, Khalid Aucho na Yacouba Songne.