>

YANGA KUWAFUATA NAMUNGO LEO

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo Jumatano, Novemba 17 wanatarajia kusepa Dar kuelekea Lindi kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC.

Vinara hao wa ligi wakiwa nafasi ya kwanza na pointi 15 Novemba 20 watatatupa kete yao ya sita kwa kusaka ushindi mbele ya Namungo itakuwa Uwanja wa Ilulu.

Yanga inatarajiwa kukutana na ushindani mkubwa kwenye mchezo huo kwa sababu mchezo wa Namungo uliopita walinyooshwa bao 1-0 dhidi ya Simba hivyo hasira za Namungo itakuwa ni kwenye kusaka ushindi.

Kwa upande wa Yanga wao watakuwa na hesabu za kuendelea na kasi ambayo wameanza nayo na mchezo wa mwisho walishinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mkapa.

Mabao yalifungwa na Feisal Salum, Djuma Shaban na Tonombe Mukoko na lile la Ruvu Shooting mfungaji alikuwa ni Shaban Msala.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wachezaji wapo tayari na wanatarajia kuanza safari leo kuelekea Lindi.

“Kama ambavyo tumemaliza mechi zetu tano ambazo zimepita kwa ushindi ndivyo ambavyo tunataka iwe hivyo kwa mechi zetu ambazo tutacheza ikiwa ni pamoja na ule dhidi ya Namungo,” amesema.

Kwenye msimamo Namungo ipo nafasi ya 11 na pointi zake ni tano.