WACHEZAJI wa Simba wameketishwa kikao na Kocha Mkuu, Pablo Franco, raia wa Ufaransa na kuambiwa kwamba wanapaswa kuonyesha uwezo wao wote walionao huku wakipigwa marufukuku mipira ya butuabutua.
Kwenye mazoezi ambayo waliyafanya jana Uwanja wa Boko Veteran Pablo alionekana kuwa mkali kwa wachezaji watakaobutua huku akiwataka wacheze soka la utulivu.
Mabingwa hao watetezi wana kibarua cha kufanya vizuri ndani ya ligi pamoja na Kombe la Shirikisho katika mashindano ya kimataifa jambo ambalo linafanya maandalizi yao yawe kwenye uangalizi mkubwa.
Tayari wachezaji wote ambao walikuwa kwenye timu ya taifa ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Aishi Manula, Shomari Kapombe wameungana na wachezaji wengine ikiwa ni pamoja na Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu kwa ajili ya mazoezi ya pamoja.
Hitimana Thiery, Kocha Msaidizi wa Simba amesema kuwa kila kitu kinakwenda sawa na wachezaji wanazidi kupewa mbinu ili kuwa imara.
“Kwa muda huu ambao ligi imesimama ni wakati wetu kuwapa wachezaji mbinu na kwa namna ambavyo ushindani umekuwa mkubwa basi tuna amini kwamba kuna jambo litatokea kwa kuwa kila mchezaji yupo tayari,” amesema Hitimana.