JURGEN Klopp, Kocha Mkuu wa Liverpool kwa sasa anapasua kichwa namna ya kuweza kuendelea kuwa kwenye ushindani kutokana na wachezaji wake nyota wa kikosi cha kwanza kuumia ikiwa ni pamoja na winga matata, Sadio Mane raia wa Senegal.
Mane aliumia kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Togo na hakuweza kuyeyusha dakika zote 90 kwa kuwa alifanyiwa mabadiliko mapema tu dakika ya 23 kwenye mchezo huo.
Pia nyota wake mwingine ambaye naye ni majanga ni mshambuliaji wake Roberto Firmino huyu tayari hayupo kambini na kikubwa ambacho kinamsumbua ni maumivu ya nyama za paja.
Klopp ana kibarua kikubwa cha kuweza kuanza kwenye mechi zijazo bila uwepo wa nyota hao kwa kuwa baada ya kunyooshwa kwa kufungwa mabao 3-2 dhidi ya West Ham United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England kituo kinachofuata ni Novemba 20 itakuwa dhidi ya Arsenal ambayo gari limewaka.