>

AJIBU,MKUDE WAONGEZEWA DOZI SIMBA

KOCHA mpya wa Simba, Pablo Franco ambaye ametua leo Novemba 10 alikuwa anawasiliana na benchi la ufundi la Simba ambalo lilikuwa chini ya Hitimana Thiery na Seleman Matola kuhusu suala la mazoezi ya vijana hao.

Taarifa zimeeleza kuwa wakati Simba wakiendelea na mazoezi kabla hajatua tayari alikuwa ametuma program ambazo zinapaswa kuanza kutumika jambo ambalo lilifanya dozi ya mazoezi kuongezwa kwa mastaa wa timu hyo ikiwa ni pamoja na Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude, Gadiel Michael na Beno Kakolanya ambao hawajaitwa kwenye timu ya taifa.

“Kocha alipokuwa nchini Hispania tayari alikuwa akifanya mawasiliano na benchi la ufundi kwa kuwasiliana na kocha msaidizi wake pamoja na uongozi wa timu kwa ajili ya kuiandaa timu.

“Timu imekuwa ikifanya mazoezi asubuhi na jioni kwa ajili ya kujiweka sawa na mechi zake zijazo na kazi ilianza Jumatatu kwa ajili ya kuendelea na mazoezi,” ilieleza taarifa hiyo.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu kuhusu maandalizi ya timu hiyo alisema kuwa maandalizi yanakwenda vizuri baada ya timu kuingia kambini.

“Tangu timu imeingia kambi ilianza mazoezi ya gym asubuhi na jioni tukafanya uwanjani ili kurudisha utimamu wa mwili kwa wachezaji baada ya kupewa mapumziko ya siku nne,” amesema.

Chanzo:Championi.