SIFA ZA KOCHA MPYA SIMBA

WAKATI majina mbalimbali ya makocha yakihusishwa kwenda kurithi nafasi ya Didier Gomes ndani ya Simba, mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu ametaja sifa za kocha wanayemtaka.

 

Mangungu alisema kwa kipindi ambacho wanapitia hivi sasa, wanahitaji kocha ambaye atakuwa tayari kukubaliana na changamoto na kubadili upepo kwa haraka ndani ya timu hiyo.

 

Mangungu aliongeza kuwa, Simba ni kubwa na imepokea maombi na CV za makocha wenye majina makubwa na mafanikio ila wamekuwa watulivu kwenye kujua nani atakuwa mtu sahihi.

Miongoni mwa majina ambayo yanatajwa kutua kwenye meza za vigogo wa Simba ni Luiz Antonio Nizzo.Kocha huyo raia wa Brazil, amewafundisha mastaa wengi kutoka nchi hiyo wanaocheza timu kubwa Ulaya kwa sasa ambao ni Alisson (Liverpool), Marcelo (Real Madrid), Casemiro (Real Madrid), Philipe Coutinho (Barcelona) na Neymar (PSG).

Akizungumza na Spoti Xtra, Mangungu alisema: “Tunahitaji kocha bora ambaye atakuja kutupa kitu ambacho Wanasimba tunakihitaji, kocha ambaye ni mzoefu na soka la Afrika, maombi yapo mengi sana lakini tumeamua kuwa watulivu kwa sasa.

 

Kwa sasa Simba inanolewa na Hitimana Thiery akisaidiana na Suleiman Matola, huku mchakato wa kumsaka kocha mkuu ukiendelea.Mbali na Mbrazil huyo, pia yupo mwingine kutoka nchini humo aitwaje Leonardo Neiva na Mjerumani, Josef Zinbbauer.