KIKOSI cha Yanga kimeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa leo Novemba 2,2021.
Alikuwa ni Shaban Msala alipachika bao kwa Ruvu Shooting dakika ya 8, kwa shuti kali akiwa nje ya 18 lililompoteza mazima kipa namba moja Djigui Diarra.
Kipa Mohamed Makaka aliweza kuwa imara kwenye dakika 20 za mwanzo kwa kuwa aliokoa shuti lililopigwa na Yacouba Songne ambaye alipata majeraha baadaye na kutoka kwenye mchezo huo.
Dakika ya 24, ya mchezo nahodha wa Ruvu Shooting Santos Mazengo alipata kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele nje ya eneo la 18.
Kocha wa Ruvu Boniface Mkwasa alifanya mabadiliko ya kumtoa Marcel Kaheza na kumuingiza beki Ally Mtoni ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ulinzi.
Mshambuliaji wa Yanga Yacouba Sogne alipata majeraha na kushindwa kuendelea na mchezo huku nafasi yake ikichukuliwa na Saido Ntibanzonkiza.Yanga iliendelea kulishambulia lango la Ruvu Shooting ambapo dakika ya 32, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliipatia Yanga bao la kusawazisha baada ya kupiga shuti kali nje ya 18, lililomshinda Makaka.
Dakika 45 zilikamilika kwa timu zote kutoshana nguvu ila ubao ulikuja kugeuka kipindi cha pili kilipoanza kwa Yanga kuanza kasi kuliandama lango la Ruvu.
Dakika ya 48 Djuma Shaban akaiandikia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya mwamuzi kutafsiri kuwa Ally Mtoni aliunawa mpira ndani ya 18.
Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Kibwana Shomari na kuingia David Bryson na Jesus Moloko akimpisha Farid Mussa. Dakika ya 76 Mukoko Tonombe ‘Ticha’ akapigilia msumari wa tatu dakika ya 75.
Kocha Nabi akafanya mabadiliko tena kwa kumtoa Feisal Salum Abdallah huku nafasi yake ikihukuliwa Yusuf Athuman na nafasi ya Mukoko Tonombe ikichukuliwa na Zawadi Mauya.
Kwa matokeo hayo, Yanga wanazidi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Bara wakiwa na jumla ya pointi 15 huku wakiwa wameshinda mechi zao zote tano ambazo wameshacheza mpaka sasa.