NYOTA WATATU NDO IMEISHA HIVYO AZAM FC

IMEFAHAMIKA kuwa Azam FC huenda ikaachana na wachezaji wake watatu Suire Boy, Aggrey Morris na Mudathiri Yahaya katika usajili wa dirisha dogo msimu huu.

 

Taarifa ya Azam iliyotolewa hivi karibuni ilisema kuwa wachezaji hao wameonesha utovu wa nidhamu kwa Meneja wa timu, Jackson Kakolaki, wachezaji wenzao, benchi la ufundi na viongozi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

 

Ilielezwa kuwa chanzo cha utovu wa nidhamu hiyo ni kumfuata ofisini meneja huyo na kumtolea maneno yasiyo na staha mara baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kumalizika dhidi ya Horseed FC ya Somalia.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, uongozi wa Azam upo katika hatua za mwisho za kuachana na wakongwe wa timu hiyo.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wachezaji watatakiwa kuchagua mawili aidha ni kutolewa kwa mkopo au kuondoka katika usajili wa dirisha dogo.

 

Aliongeza kuwa muda wowote kuanzia hivi sasa wachezaji hao watapewa taarifa hizo wakati Ligi Kuu Bara ikiendelea katika viwanja mbalimbali.

 

“Sure Boy, Mudathiri na Morris ngumu kurejeshwa tena katika timu kutokana na utovu wa nidhamu walioufanya kwa meneja, uongozi, benchi la ufundi na uongozi.

 

“Tayari wachezaji hao wameondolewa katika mipango ya kocha baada ya kufanya kitendo hicho cha utovu wa nidhamu.

 

“Wachezaji hao muda wowote watapewa taarifa ya kuchagua mambo mawili ambayo ni kutolewa kwa mkopo au wao wenyewe waondoke,”alisema mtoa taarifa huyo.

 

Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria hivi karibuni alithibitisha kwa wachezaji hao kusimamishwa na uongozi wa timu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu.