BAADA ya Alhamisi ya Oktoba 28 kusambaa kwa taarifa kwamba mastaa wa Yanga wamepanga kufanya mgomo kushinikiza malipo yao ya bonasi, hatimaye mambo yamewekwa sawa
na sasa ni full kicheko kwao.
Ishu ipo hivi; Alhamisi ya Oktoba 28, 2021, habari kubwa ilisomeka; “Kisa bonasi…Mastaa Yanga watangaza mgomo ilikuwa ni ndani ya Spoti Xtra Alhamisi kisha baadaye stori hiyo ikasambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya habari hiyo kutoka, iliwashtua viongozi wa Yanga, fasta wakatinga kambini na kuweka mambo sawa ili tu kuondoa sintofahamu ambayo ingeweza kuwafanya waingie kinyonge katika
mchezo wao dhidi ya Azam FC.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, baada ya viongozi kuona taarifa ile, iliwafanya kufika fasta kambini hapo na kuweka kikao kizito na mastaa hao wakitaka kujua ni nani aliyefichua siri hiyo.
“Ile habari ya mgomo ilileta balaa kubwa kambini, viongozi walikuja wakiwa na hasira kweli wakitaka kumjua nani aliyetoboa siri wakati haikutakiwa kutoka nje.Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, katika kikao hicho, mastaa hao wa Yanga walifanyiwa msako wa kutisha ili abainike aliyevujisha taarifa hizo za ukweli na uhakika, lakini hakuna aliyepatikana
“Wachezaji wote walisachiwa simu zao, lakini hakuna kilichopatikana. Mwisho wa siku wakazungumza nao kirafiki na kuweka mambo sawa.
“Baada ya kikao cha kwanza kufanyika Alhamisi, Ijumaa wakaja tena kuongeza hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Azam ambapo walitoa ahadi kama kawaida yao na kutoa ile bonasi ya mechi mbili kati ya tatu walizotakiwa kutoa.
“Bonasi iliyotoka ni ya mechi dhidi ya Geita Gold na KMC ambazo jumla ni shilingi milioni 40 kwa maana ya kila mechi bonasi ya ushindi ni shilingi milioni 20, ile ya Simba ambayo bonasi yake shilingi milioni 400, wachezaji wameahidiwa watapewa Jumatatu baada ya kumalizana na Azam.
“Baada ya kikao hicho, tabasamu pana kwa wachezaji likaibuka na wakaahidi kutofanya mgomo, huku wakipania kufanya kweli kwenye kila mechi ili kufikia malengo ya kubeba ubingwa msimu huu,” kilisema chanzo
hicho.
Kwenye mchezo wao dhidi ya Azam FC, Yanga ilishinda mabao 2-0 na watupiaji walikuwa ni Jesus Moloko na Fiston Mayele.