LICHA ya kwamba ameshabwanga manyanga ndani ya kikosi cha Simba, Didier Gomes raia wa Ufaransa kuna mechi nyingi ambazo alizishuhudia kwake zilikuwa ni za moto na pasua kichwa kwa namna wachezaji wake walivyopambana na mwisho kupata matokeo ama kuangukia pua.
Hizi ni Mechi 5 ambazo ni dakika 450 zilizokuwa ni za moto kwa Gomes alipokuwa ndani ya Simba inayopambana kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara:-
Simba 3-0 Kaizer Chiefs
Ilikuwa ni Mei 22, Uwanja wa Mkapa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ikiwa kwenye ule ubora wake iliweza kushinda mabao 3-0 ila safari iliishia hapo katika hatua ya robo fainali kwa kuwa walikuwa na mzigo wa mabao 4-0 waliyopewa walipowafuata wapinzani wao Kaizer Chiefs kule Afrika ya Kusini.
Simba 0-1 Yanga
Juali 3, acha kabisa kuambiwa kuhusu Simba na Yanga, wakati ule Haji Manara akiwa ni Ofisa Habari wa Simba aliwaaminisha mashabiki wa Simba kwamba watashinda kwa namna yoyote ile huo mchezo ila moto uliwaka Uwanja wa Mkapa.
Lilipigwa mbungi kali sana mwisho Yanga ilishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara na mtupiaji alikuwa ni kiungo Zawadi Mauya ambaye ni mzawa.
Azam FC 0-1 Simba
Ilikuwa ni hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, Uwanja wa Majimaji, Songea ngoma ilipigwa mpaka jioni kabisa Simba ilipata ushindi kwa bao lililopachikwa na kiungo Luis Miquissone akitumia faulo iliyoanzishwa harakahara na Bernard Morrison.
Simba 1-0 Yanga
Julai 25 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho na ilikuwa ni fainali ya moto iliyochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika kule mwisho wa reli Kigoma kati ya Simba v Yanga na ulipigwa mpira mkubwa kwa timu zote.
Baada ya dakika 90 kukamilika ubao ulisoma Simba 1-0 Yanga na bao la ushindi kwa Simba lilifungwa na Taddeo Lwanga kwa pasi ya mshikaji wake Luis Miquissone ambaye alipiga pigo la kona likakutana na kichwa cha mtupiaji.
Simba 1-3 Jwaneng Galaxy
Hapa mwendo ulikuwa umebadilika hakuwa na furaha kwenye mchezo wake wa mwisho Oktoba 24,2021 licha ya kwamba alikuwa kwenye jukwaa jukumu lake ilikuwa ni kuona timu inashinda mwisho wa siku wachezaji wakazingua kwa kushindwa kulinda ushindi walioupata ugenini wa mabao 2-0 na kumfanya kocha huyo aamue kubwaga manyanga.
Kwa sasa Simba ipo chini ya kocha Hitimana Thiery ambaye yupo hapo kwa muda na amekiongoza kikosi hicho kwenye mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania na timu hiyo ilishinda bao 1-0.