>

ANSU ANAAMINI HAWEZI KUMFIKIA MESSI

KINDA wa Barcelona, Ansu Fati amesema kuwa alipata ofa nyingi sana lakini akaamua kubaki Barcelona na wala hana wasiwasi kuvaa jezi ya Lionel Messi.

Fati alikubali kusaini mkataba mpya wa miaka sita na Barcelona na sasa dau lake la usajili ni Euro bilioni moja jambo ambalo linaonekana kuishtua dunia.

 

Kinda huyo ambaye anatajwa kuwa anatakiwa kuwa maarufu kama Lionel Messi amesema kuwa alipata ofa nyingi sana kabla hajakubali kusaini mkataba huo na timu kadhaa zinatajwa kuwa zilimwania ikiwemo Man United, Liverpool na Chelsea.

 

“Kulikuwa na ofa nyingi sana kabla sijakubali kusaini kuitumikia Barcelona tena kwa kipindi cha miaka sita, lakini awali nilishamwambia wakala wangu Jodes Mendes kuwa nabaki hapa.

“Hapa ni sehemu muhimu sana kwangu na naona fahari sana kuendelea kubaki hapa, sifikiri kuhusu jambo lingine kwa sasa baada zaidi ya kuisaidia Barcelona iweze kuwika Ulaya na duniani kwa ujumla,” alisema Fati.

 

Hata hivyo, kinda huyo amesema hana haja ya kufananishwa na Lionel Messi kwa kuwa anaamini kuwa yeye anatakiwa kufuata njia yake mwenyewe.

Mara baada ya kusaini mkataba huo mrefu Barcelona walimpa kinda huyo jezi namba kumi ambayo alikuwa akiivaa Messi na mwenyewe alisema hana presha hata kidogo kutokana na ukubwa wa jezi hiyo.

 

“Sina presha hata kidogo, sijali jambo lolote naamini kuwa Lionel Messi alikuwa na staili yake nami nina staili yangu.

“Kabla ya kukubali kubaki hapa nilijaribu kupata ushauri kutoka sehemu mbalimbali na suala la kubaki linaonekana kuwa sahihi zaidi.

 

“Lionel Messi alikuwa bora kwa kipindi kirefu sana hapa, nafikiri jambo la msingi ni mimi kufuata staili yangu mwenyewe,” alisema kinda huyo.

Fati, ambaye mwisho wa mwezi huu anatimiza miaka 19 amesema kuwa aligoma kwenda kujiunga na timu kadhaa za England kwa kuwa aliona kuwa Barcelona ni sehemu muhimu zaidi kwake kwa sasa.

 

“Kwangu mimi naamini hapa Barcelona hakuna ambaye atakuja kuwa kama Lionel hakuna ambaye atakuja kuwa kama Carles Puyol au Xavi Hernandez.

“Siamini kama kuna mtu atafikia kiwango ambacho aliwahi kufikia Messi hapa, bado sijafanya jambo lolote lile kubwa nafikiri natakiwa kusubiri kuweka rekodi zangu hapa.

 

Fati ambaye anaaminika kuwa atakuwa mchezaji mahiri miaka kadhaa ijayo amefanikiwa kufunga mabao 15 kwenye michezo 48 ambayo ameshaitumikia Barca kwa sasa.

Fati, alijiunga na Barcelona miaka 10 iliyopita akitokea kwenye kikosi cha Sevilla mwaka 2012.

 

Fati ni mzaliwa wa Guinea Bissau lakini alikubali kuitumikia timu ya Taifa ya Hispania ambayo bado hajapata nafasi sana kutokana na umri wake.

Amefanikiwa kuitumikia Hispania kwenye michezo minne tu na kufunga mabao mawili, lakini anaaminika kuwa anaweza kuwa bora zaidi kwenye timu hiyo miaka kadhaa ijayo.

 

Katika maisha yake ya soka hadi sasa amefanikiwa kutwaa tuzo moja ya mchezaji bora wa mwezi wa La Liga na kufanikiwa kutwaa Kombe la Copa del Rey akiwa na Barcelona.