>

RAIS SAMIA AWAPA VIWANJA WACHEZAJI WA TWIGA STARS

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewapatia viwanja jijini Dodoma wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Twiga Stars kwa kuibuka mabingwa wa COSAFA 2021.

Rais Samia (katikati) akiwa na baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars na viongozi mbalimbali.

Rais Samia ametoa zawadi hiyo leo Oktoba 27, 2021 alipowaalika kwaajili ya kupokea kombe hilo pamoja na kupata chakula cha mchana.

”Nitawapatia watoto wangu wa Twiga Stars Viwanja vya kujenga nyumba zao, vitakuwa kule Dodoma ambako na mimi mama yenu naishi,” amesema Rais Samia Saluhu.

Aidha amesisitiza kuwa soka la wanawake linatakiwa kupewa kipaumbele kama ilivyo kwa upande wa wanaume.

”Soka la wanawake limeanza miaka ya hivi karibuni lakini mafanikio yenu yameanza kuwatetemesha wanaume. Mimi huwa nasema timu ya wanawake imefanya vizuri mara kadhaa lakini hakuna anayesimama kuwasifu, lakini wanaume wakishinda tu nusu fainali sifa zinapasua anga,”.