MAMBO ni magumu kwenye benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Kocha Mkuu, Didier Gomes ambapo inaelezwa kuwa muda wowote ule wanaweza kuchimbishwa.
Mpaka wakati huu makocha wa timu hiyo ikiwa ni Gomes pamoja na Hitimana Thiery ambaye ni kocha msaidizi wa timu hiyo hawajui hatma yao kama wataendelea kubaki ama la.
Ilikuwa ni Oktoba 24 mambo yalibadilika baada ya ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 1-3 Jwaneg Galaxy na timu ya Simba ambao walikuwa ni wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho.
Habari zimeeleza kuwa kwa sasa makocha hao wameyeyusha furaha baada ya viongozi wa Simba kutoa kauli ambazo ni mbaya kwao kwa ajili ya kupiga kazi ndani ya Simba.
“Kiukweli kwa sasa makocha wapo kwenye hali mbaya na hawajui nini kimesababisha kupoteza mchezo huo, imekuwa ni presha kubwa kwa wakati huu kwa kila mmoja.
“Pia kauli ya Mo na Crescentius Magori hizi zimeharibu kabisa hali ya hewa ndani ya Simba,” ilieleza taarifa hiyo.
Mo alibainisha kuwa wale ambao wamehusika kwa kupoteza kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika lazima wachukuliwe hatua.