>

HAJI MANARA:TUMEJIPANGA KUSHINDA MBELE YA AZAM

HAJI Manara, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanaamini mchezo wao dhidi Azam FC unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 30 utakuwa na ushindani mkubwa ila wamejipanga kupata pointi tatu muhimu.

Akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Serena Hotel, Manara amesema kuwa wanatambua mchezo utakuwa na ushindani kwa kuwa wanakutana na timu imara.

“Tunao mpango wa kufanya vizuri kwenye mechi zetu ikiwa ni pamoja na hii ijayo dhidi ya Azam FC ambapo lengo kubwa ni kupata pointi tatu muhimu huku tukiwaheshimu wapinzani wetu na tupo tayari.

“Kikubwa ni kwamba kila kitu kinakwenda sawa na kutakuwa na mambo ya tofauti kidogo, tunao wachezaji wazuri na wapo tayari kwa ajili ya ushindani,

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kwa kuwa ipo wazi kwamba hapa nilipo Yanga hakuhitaji kutumia nguvu nyingi badala yake ni suala la kuwakumbusha tu mashabiki ili wajitokeze,” amesema.

Yanga ipo na pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu na kukusanya pointi hizo inakutana na Azam FC ambayo imetoka kufungashiwa virago kwenye Kombe la Shirikisho kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Pyramids nchini Misri.