KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amesema kuwa wachezaji wake, Mghana Bernard Morrison na Mkongomani, Heritier Makambo, wana kazi maalum za kimbinu na kiufundi katika kikosi chake.
Nabi amesema kuwa wachezaji hao anawatumia kama ‘Super Sub’ ambao kazi yao ni kwenda kuwazuia mabeki na viungo wakabaji wa timu pinzani kupanda.
Nabi amesema kuwa anapenda kuwatumia wachezaji hao katika kipindi cha pili katika dakika za mwishoni kwa lengo la kuwachosha mabeki na viungo wakabaji wa wapinzani wao kutegemeana na aina ya mchezo..
Aliongeza kuwa alianza kuwatumia katika mchezo wa Wiki ya Mwananchi waliocheza dhidi ya Vipers United ya Uganda, Kariakoo Dabi na ule wa Polisi Tanzania ambao mabeki na viungo wa timu pinzani walikuwa nyuma wengi wakilinda.
“Mchezo wetu dhidi ya Polisi Tanzania ulikuwa mgumu kutokana na mabeki na viungo wakabaji kukaa golini wengi wakilinda goli lao na hasa katika kipindi cha pili.
“Baada ya kuona mambo yanakuwa magumu nikachukua maamuzi ya kumuingiza Makambo ambaye kazi yake ilikuwa ni kuwazuia mabeki na viungo wa timu pinzani wasipande kuja kutushambulia na badala yake tuwashambulie wao.
“Pia nikamuingiza Morrison ambaye yeye naye aliongeza kasi ya ushambuliaji kabla ya kupiga asisti yake iliyozaa bao la pili. Pia kuingia kwake kuliwafanya mabeki wa timu pinzani kujaa presha kubwa kutokana na kiwango chake alichonacho,” amesema Nabi..
Wawili hao kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union walianza kikosi cha kwanza wakati timu hiyo iliposhinda mabao 2-0 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.