STARS KAZI NI KWENU KUWAPA RAHA MASHABIKI

MAANDALIZI yamezidi kupamba moto kwa wachezaji 27 ambao waliitwa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen kwa ajili ya kuanza kujipanga kwa mechi za kimataifa ambazo ni ngumu na muhimu kupata ushindi.

Kwa hilo kinachotakiwa kwa wale ambao wameitwa katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni kuwapa raha mashabiki ambayo ni ushindi hakuna namna nyingine.

Kuwa kwenye orodha ni jambo moja na kutimiza yale ambayo yapo kwenye orodha ni jambo la msingi kwa sababu Watanzania wanapenda kuona matokeo chanya yanapatikana.

 

Novemba 11 wala sio mbali itafika na ipo wazi kwamba siku hazingandi. Kwa muda uliopo kwa sasa licha ya kwamba muda ni mfupi bado kuna umuhimu wa kufanya linalowezekana kwa ajili ya kupata ushindi mbele ya DR Congo ili kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Kombe la Dunia.

 

Mechi mbili zijazo ni ngumu na zanguvu nyingi pamoja na akili.Suala la kuongoza kundi kwa sasa hilo hata lisipewe kipaumbele kwa sababu kuna wakati timu ilikuwa inaongoza ila ikapoteza mchezo wake ikiwa nyumbani jambo ambalo liliwaumiza Watanzania wengi.

 

Ikumbukwe kwamba tulipoteza mbele ya Benin tukiwa nyumbani hapo tusijisahau kazi ipo mbele yetu ni kubwa.

 

Ukweli ni kwamba kwenye mchezo wa mpira hakuna suala la kutabiri matokeo hivyo hilo likae kwenye vichwa vya wachezaji pamoja na mashabiki wote.

 

Mchezo dhidi ya DR Congo pamoja na ule dhidi ya Madagascar yote ni migumu hakuna mchezo hata mmoja ulio mwepesi jambo la msingi ni maandalizi mazuri.

 

Tayari wachezaji wameanza mazoezi na kufanya maandalizi basi jitihada za kweli zinahitajika kwenye mechi zote.

 

Imani kwa wachezaji ni kubwa na kila mmoja anajua kwamba utamaduni wa Watanzania ni kuwa bega kwa bega na timu kwenye maumivu pamoja na furaha.

 

Kuwa kwenye kikosi kinachocheza mechi za kimataifa ni fursa na soko kwa wale ambao watajituma kwa kuwa dunia inafuatilia michezo na vipaji havifichiki.

 

Hivyo kwa namna ambavyo wachezaji watajituma na kufanya kweli kwenye mechi hizo za kimataifa itawafanya waingie kwenye soko la kimataifa katika suala la kupata timu nje ya nchi.

 

Ili hayo yote yatokee ni jambo moja tu linatakiwa wachezaji kucheza kwa juhudi isiyo ya kawaida na kutimiza majukumu yao kwa umakini.

 

Umakini kwenye kutengeneza nafasi ni jambo la kwanza na katika kumalizia pia ni jambo la mwisho ambalo linahitajika kwenye kila mchezo ambao utachezwa.

 

Yote kwa yote tunaamini kwamba wachezaji mtawapa furaha mashabiki na furaha yao imebebwa na jambo moja tu ushindi hakuna jambo lingine zaidi ya hilo.