>

KOCHA WA SIMBA KUJA NA MASHINE MPYA

IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco anahitaji kuja na watu wake wa kazi kwa ajili ya kupata matokeo chanya kwenye mechi zake ambazo atacheza.

Pablo ambaye amepewa dili la miaka miwili anatarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa baada ya kutangazwa kuwa mrithi wa mikoba ya Didier Gomes ambaye alibwaga manyanga.

Habari kutoka kwa mtu wa ndani wa Simba imeeleza kuwa kocha huyo anatambua kwamba panga limepita Simba kuanzia kwenye eneo la kocha wa viungo pamoja na yule wa makipa jambo ambalo linamfanya afikirie kuja na watu wapya wa kazi.

“Suala la kuleta wachezaji na makocha kwa Simba huwa linakuwa mikononi mwa viongozi lakini kuna ushauri na kuzungumza na kocha ambaye amechaguliwa hivyo naye huwa anakuwa na mapendekezo yake.

“Ambacho anakihitaji kocha kwa sasa ni kuwa na benchi kamili hivyo mchakato unaendelea kuona namna gani inaweza kuwa mambo yakikamilika itafahamika kama atakuja naye yeye ama atawakuta lakini hata akija naye yeye ni lazima afanye mawasiliano na viongozi kisha mchakato ufanye kazi,” ilieleza taarifa hiyo.

 

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Simba,Murtaza Mangungu alisema kuwa mchakato wa kusuka benchi la ufundi unaendelea.