RUVU YAPANIA KUTIBUA REKODI YA YANGA KWA MKAPA

KUELEKEA mchezo wa leo dhidi ya Yanga, Ruvu Shooting wamefunguka kuwa watatibua rekodi ya Yanga ya kutofungwa kwenye mechi walizocheza kwa msimu huu.

 

Saa 12:15 leo Yanga wanatarajiwa kuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya Ruvu Shooting mchezo ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki na wapenda burudani.
Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting,Rajab Mohamed amesema kuwa wanatambua namna watakavyoweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo kwa kuwa maandalizi yapo kamili.
 “Tunamshukuru Mungu tupo vizuri, tumejiandaa vizuri kuvunja rekodi ya Yanga kwa msimu huu ya kucheza bila kufungwa kwenye mechi zao ambazo wamezicheza mpaka wakati huu.
“Hatuna majeruhi kwenye kikosi chetu wachezaji wote wapo sawa, kikubwa ni kupata matokeo kwenye mchezo wetu wa leo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona burudani.
“Tunajua kuwa Yanga hawajawahi kupoteza mchezo wowote ila sisi tutakuwa wa kwanza kwani tumeona michezo yao minne waliyocheza na tumeona madhaifu yao hivyo tutapata matokeo,” .
Kwa upande wa nahodha wa Ruvu Shooting, Ambrose Morris amesema:-“Maandalizi yote yamekamilika hivyo tuna uhakika wa kushinda mchezo huo kwa asilimia nyingi.”