WALIFANYA POA ILA HAWAKUTAJWA KWENYE ORODHA YA TUZO

WAPO watu leo wengine watakuwa kwenye mnuno wa kishkaji kwa kushindwa kusepa na tuzo katika sherehe iliyofanyika Ukumbi wa kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere,(JNICC) ambapo tuzo zitatolewa huku wengine wakiwa na furaha baada ya kusepa na tuzo hizo.

 

Kwenye tuzo hizo kuna baadhi ya mastaa ambao walifanya kazi nzuri ila kutokana na ushindani kuwa mkubwa, majina hayakuweza kutokea katika orodha ya wale wanaowania tuzo kwenye upande wa ligi na badala yake wameshuhudia washkaji zao wakisepa na tuzo na kujifunza jambo kwao:-

 

Mshery

 

Aboutwalib Mshery, kipa namba moja wa Mtibwa Sugar alikuwa kwenye ubora wake msimu wa 2019/20 na aliweza kukusanya jumla ya clean sheet 13 jambo ambalo linaamanisha kwamba yupo imara katika eneo la kazi.

 

Hana bahati kwa kuwa watasikiliza tu na kutazama nani ataibuka mbabe leo kati ya Aishi Manula wa Simba, Jeremia Kisubi ambaye alikuwa anakipiga ndani ya Tanzania Prisons na sasa yupo Simba pamoja na Haroun Mandanda mali ya Mbeya City.

 

Mzamiru Yassin

 

Yupo zake ndani ya Simba hana makuu sana ila ni mtu wa kazi chafu, jina  lake halipo kwenye orodha ya viungo wanaowania tuzo lakini kazi yake haikuwa haba kwa msimu wa 2019/20.

 

Kwa eneo lake la ukabaji alikuwa akiwafungulia njia viungo wengine ambao walikuwa wakiibuka nyota katika mchezo ikiwa ni pamoja na Luis Miquissone, Clatous Chama ambaye yupo kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo.

 

Idd Suleiman

 

Yupo zake ndani ya Azam FC kiungo huyu fundi mhimili kwenye eneo la kati na ni moja ya wenye namba za bahati wawapo ndani ya uwanja.

 

Mabao yake kibindoni ni 9 na alitoa jumla ya pasi 7 hivyo sio mtu wa kubeza akiwa uwanjani ila hana namna ana kazi ya kuongeza juhudi zaidi ili wakati ujao jina lake liwepo pia.

 

Luis Miquissone

 

Kiungo namba mbili kwa pasi za mwisho ndani ya Simba kwa msimu uliopitia wa 2019/20 ambapo alikuwa nazo 10 na alitupia mabao 9. Kinara ni Chama ambaye alitoa pasi 15 na alifunga mabao 8 ila jina la Luis ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya Al Ahly ya Misri halijaingia kwenye droo apambane ikiwa atarudi tena ndani ya Simba atakuwa na nafasi ya kupenya. Wanaowania tuzo ni Clatous Chama aliyekuwa anakipiga Simba,Mukoko Tonombe na Feisal Salum wapo Yanga.

 

Chris Mugalu

 

Jina la Mugalu halina bahati katika kipengele chochote licha ya kuwa ni namba mbili kwenye utupiaji ambapo alifunga mabao 15 na kinara ni John Bocco. Hii inamaanisha kwamba hasira zake za kutokuwa katika wale wanaowania tuzo kutamfanya aongeze juhudi msimu huu wa 2020/21.

 

Prince Dube

 

Nyota mmoja matata sana kwenye usajili ambao Azam FC walibonyeza kitufe kikakajibu basi hapa wanastahili pongezi.

 

Ninja anatupia kisha anaachia tabasamu, majeraha yamemfanya agote kwenye mabao 14 na pasi zake tano ila jina lake halipo kwa wale wanaowania tuzo maana yake ni kwamba ligi ya Bongo sio ya mchezomchezo.

 

Joash Onyango na Pascal Wawa

 

Safu yao ya ulinzi ni namba moja kwa kuruhusu mabao machache katika mechi 34 ambayo ni 14 na hawa walikuwa ni viongozi.Majina yaliopo kwa wanaowania tuzo ni Mohamed Hussein na Shomari Kapombe kutoka Simba pamoja na Dickosn Job wa Yanga.

 

Wapo wachezaji wengi ambao leo watashuhudia tuzo zikitolewa na imani ni kwamba kutokuwepo kwao itakuwa ni darasa ili waweze kuongeza juhudi zaidi na kama kuna makosa ambayo yatakuwa yamefanyika na waandaaji itakuwa sehemu ya kujifunza pia.