WAWAKILISHI WETU KIMATAIFA KAZI IPO KWENU

    KUPATA nafasi ya timu nne kushiriki katika mashindano ya kimataifa kunahitaji matokeo mazuri kwa wawakilishi wetu wa kimataifa ambao wana kazi ya kupeperusha bendera.

    Kufanya kwao vizuri kwenye mechi za mwanzo ni hatua nzuri na inaongeza nguvu ya kupambana kwenye mechi zijazo kwa sababu wamepata sehemu ya kuendelea pale ambapo walikuwa wameishia.

    Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara walianza ugenini kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana katika hilo wanastahili pongezi.

    Ushindi wao ni furaha kwa taifa na mashabiki wa Simba kiujumla huku ikionekana kwamba wamezidi kuwa imara kwenye mechi za kimataifa.

    Malengo yao wameweka wazi kwamba wanahitaji kutinga hatua ya nusu fainali ila wakumbuke kwamba msimu uliopita walifanya makosa yaliyoharibu ndoto yao ya kuweza kufika hapo.

    Kukumbuka makosa waliyoyafanya msimu uliopita sio suluhisho la matatizo bali wanatakiwa wayakumbuke na kuyafanyia kazi.

    Maisha yanakwenda kasi na kila siku mbinu zinabadilika. Ni wakati mwingine wa kufanya vizuri kwenye mechi ya marudio ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya makundi.

    Kumaliza kazi ugenini ilikuwa sehemu ya kwanza ya ushindi sehemu ya pili ni nyumbani hapo lazima mmalize kazi kwa uzuri kwani inawezekana.

    Kwa kuwa mbinu zenu wakati huu zipo mikononi mwa wapinzani wenu basi fanyeni kazi ya ziada kusaka ushindi nyumbani.

    Ulimwengu wa mpira kwa sasa mambo yamebadilika na kila mmoja ana nafasi ya kushinda ugenini hata nyumbani kwa namna yoyote ile.

    Jambo la msingi ni kuongeza juhudi na kufanya mbinu mpya ambazo zitawapa matokeo. Imani yangu ni kwamba wachezaji wanatambua uzuri wa mashindano ya kimataifa.

    Mbali na wachezaji hata benchi la ufundi pia linatambua umuhimu wa mashindano ya kimataifa. Hapa ni sehemu pekee inayowaweka wachezaji kwenye ramani pamoja na benchi la ufundi kwenye kuongeza CV.

    Biashara United na Azam FC pia ni wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho pia bado kazi ipo ambapo kwenye mechi zao zilizopita kila mmoja amepata matokeo yake.

    Hawa wa kwenye Kombe la Shirikisho wao watakuwa ugenini kwa kuwa mechi za mwanzo walicheza nyumbani, Azam ililazimisha sare mbele ya Pyramids bila kufungana na Biashara United ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly Tripol ya Libya.

    Kila mmoja ana kazi ya kupeperusha bendera kimataifa inawezekana.

    Previous articleKIKOSI BORA CHA LIGI YA WANAWAKE TANZANIA
    Next articleWALIFANYA POA ILA HAWAKUTAJWA KWENYE ORODHA YA TUZO