YANGA WATUPA DONGO KIMTINDO SIMBA KISA KICHAPO

BAADA ya wawakilishi wa kimataifa katika Kombe la Shirikisho, Simba kufungwa 3-0 dhidi ya ASEC Mimosas watani zao wa jadi Yanga wametupa jiwe gizani kimyakimya.

Kupitia Insta yao waliachia picha ya Djuma Shaban akiwa mwenye kicheko na kuuliza..wawakilishi wa nini..au basi…

Haji Manara Ofisa Habari wa Yanga aliweza kudondosha maoni yake kwa kuandika labda wawakilishi wa kucheza baikoko.

Kupoteza kwa Simba kunaifanya iporomoke kimataifa kutoka nafasi ya kwanza mpaka nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi zake ni zilezile 7.

Vinara sasa ni ASEC ambao wana pointi 9 kibindoni na nafasi ya pili ni mali ya RS Berkane ambao nao bado hawana uhakika wa kutinga hatua ya robo fainali mpaka watakaposhinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya ASEC Mimosas ambao nao wanahitaji nafasi hiyo.

Kwa Simba wao kibarua chao ni kusaka ushindi mbele ya USGN ya Niger kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Aprili 3.