Paul Makonda amesema alimwomba mchezaji wa zamani wa England national football team na klabu ya Manchester United FC, Rio Ferdinand, kutoposti kwa sasa kuhusu uwepo wake nchini Tanzania, akieleza kuwa jambo muhimu zaidi ni kazi ya maendeleo na kuinua vipaji vya vijana wa Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 22, 2026 jijini Dar es Salaam, Makonda alisema kumekuwa na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kwanini Rio Ferdinand hajapost kuhusu ziara yake nchini, badala ya kuangalia ajenda kuu ya maendeleo.
“Wakati mwingine tunapenda kubeza mambo lakini hatujui nguvu kubwa inayofanywa na viongozi wetu kufanikisha hayo mambo. Ajenda kubwa ilikuwa ni kwanini Rio hajapost kwenye akaunti yake kuwa yupo Tanzania,” alisema Makonda.
Aidha, Waziri huyo alieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijikita zaidi kwenye mijadala ya mitandaoni badala ya kuangalia manufaa ya muda mrefu yanayoweza kupatikana kupitia ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya michezo, vipaji na maendeleo ya vijana.
“Tunapenda kujadili mambo kwa kuyaona bila kuyajua na mwisho tunaamini tunajua kila kitu. Ulishawahi kufikiria mtu yupo anaongelea mema juu ya nchi yako, namna Serikali inavyopiga hatua, halafu wewe badala ya kuchukua ile content uipeleke duniani unataka yeye ndio apost?” alisema Makonda.
Ziara ya Rio Ferdinand nchini Tanzania imeendelea kuvuta hisia za wananchi na wadau wa michezo huku wengi wakitarajia ujio huo kuleta fursa mpya kwa vijana wenye vipaji nchini.