FEI TOTO APELEKWA ULAYA

KITASA wa zamani wa Yanga ambaye sasa anakipiga ndani ya Polisi Tanzania, Said Juma Makapu, amesema anaamini kwa kiwango alichonacho kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ni muda wake sasa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kwa kusema hivyo kitasa huyo ni kama amempeleka Ulaya kiungo huyo ambaye kwa sasa yupo kwenye ubora wake ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Fei Toto amekuwa katika kiwango bora msimu huu. Mpaka sasa amefanikiwa kuhusika kwenye mabao matatu ya Yanga, akifunga mabao mawili na kuasisti bao moja katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara pekee.

Makapu amesema: “Kwangu Feisal ni miongoni mwa viungo bora sana hapa nchini, na kwa kiwango ambacho
amekuwa akikionyesha kwa sasa, bila 
shaka anastahili kupata nafasi ya kucheza soka la kimataifa nje ya nchi.

“Jambo la msingi kwake ni kuhakikisha anafanya sana mazoezi, kumsikiliza mwalimu wake na kuomba Mungu, naamini atatimiza malengo hayo.

Makapu Jumatano alikuwa sehemu ya kikosi cha Polisi Tanzania ambacho kilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.