Ronaldo Aongoza Dunia Kwa Mapato, Messi Na Benzema Wamfuata Kwenye Orodha Ya Wanamichezo Wanaolipwa Pesa Nyingi Zaidi

Mwanasoka wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ameendelea kutawala ulimwengu wa michezo kwa upande wa mapato, akiongoza orodha ya wanamichezo wanaoingiza fedha nyingi zaidi duniani kwa mwaka 2026, kwa mujibu wa takwimu za jarida la Forbes.

Ronaldo, anayeichezea klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia, anakadiriwa kuingiza dola milioni 300 kwa mwaka, sawa na takribani Shilingi bilioni 780 za Tanzania, kupitia mshahara wake wa soka, mikataba ya matangazo, udhamini na shughuli mbalimbali za kibiashara.

Katika nafasi ya pili yupo bondia wa Mexico, Canelo Álvarez, anayekadiriwa kuingiza dola milioni 170 kwa mwaka, huku mwanasoka Lionel Messi wa Inter Miami akishika nafasi ya tatu kwa mapato ya dola milioni 140.

Nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani, LeBron James, anashika nafasi ya nne akiwa na mapato ya dola milioni 137.8, akifuatiwa na mchezaji wa baseball wa Japan, Shohei Ohtani, anayekadiriwa kuingiza dola milioni 127.6 kwa mwaka.

Nafasi ya sita inashikiliwa na Stephen Curry wa Golden State Warriors mwenye dola milioni 124.7, huku mchezaji wa gofu kutoka Hispania, Jon Rahm, akishika nafasi ya saba kwa mapato ya dola milioni 107.

Mwanasoka wa Ufaransa, Karim Benzema, anayekipiga Al-Hilal ya Saudi Arabia, anashika nafasi ya nane akiwa na dola milioni 104, akifuatiwa na Kevin Durant wa Houston Rockets mwenye dola milioni 103.8.

Akifunga orodha ya wanamichezo 10 wanaoingiza fedha nyingi zaidi duniani ni dereva wa mashindano ya magari ya Formula 1, Lewis Hamilton, ambaye anakadiriwa kuingiza dola milioni 100 kwa mwaka kupitia mikataba yake ya mbio na shughuli za kibiashara.

Kwa ujumla, orodha hiyo inaonesha namna sekta ya michezo inavyoendelea kuwa moja ya maeneo yenye mzunguko mkubwa wa fedha duniani, huku wanamichezo wakinufaika si tu na mishahara na zawadi za mashindano, bali pia mikataba ya matangazo, udhamini na uwekezaji wa kibiashara.

ORODHA YA WANAMICHEZO 10 WANAOINGIZA FEDHA NYINGI ZAIDI DUNIANI

  1. Cristiano Ronaldo (Soka) – Dola milioni 300.
  2. Canelo Álvarez (Ndondi) – Dola milioni 170.
  3. Lionel Messi (Soka) – Dola milioni 140.
  4. LeBron James (Mpira wa Kikapu) – Dola milioni 137.8.
  5. Shohei Ohtani (Baseball) – Dola milioni 127.6.
  6. Stephen Curry (Mpira wa Kikapu) – Dola milioni 124.7.
  7. Jon Rahm (Gofu) – Dola milioni 107.
  8. Karim Benzema (Soka) – Dola milioni 104.
  9. Kevin Durant (Mpira wa Kikapu) – Dola milioni 103.8.
  10. Lewis Hamilton (Formula 1) – Dola milioni 100.

 

**CHANZO: FORBES**