Kocha wa Manchester United, Michael Carrick, amesema licha ya matokeo mabaya ambayo timu yake imekuwa ikiyapata, anaisubiri kwa hamu mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya AS Roma itakayochezwa Jumanne katika Uwanja wa Old Trafford.
Manchester United inaingia kwenye mchezo huo ikiwa haijapata ushindi katika mechi tisa mfululizo kwenye mashindano yote, rekodi mbaya zaidi kwa klabu hiyo tangu msimu wa 1988/89.
United haijawahi kucheza mechi 10 mfululizo bila ushindi ndani ya msimu mmoja tangu msimu wa 1977/78. Hali hiyo imeongeza presha kwa Carrick, huku kukiwa na hisia zinazoongezeka kuwa anaweza kupoteza kazi yake wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kwa upande wa Roma, kipigo pekee ilichopata msimu huu kilikuwa dhidi ya Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa mwezi uliopita, ambapo iliongoza mabao 3-1 kabla ya kuruhusu wapinzani kusawazisha na kushinda zikiwa zimesalia dakika saba pekee.
Manchester United inashika nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu England, huku ikishuka hadi nafasi ya 21 katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa baada ya kucheza mechi tatu, kufuatia vipigo dhidi ya Atletico Madrid na Como. Ni timu 24 za juu zitakazofuzu hatua inayofuata.
Akizungumzia mchezo huo, Carrick amesema licha ya mazingira magumu yanayoizunguka timu yake, anaamini mchezo huo ni nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa msimu wao.
“Unaweza kufikiri nina wazimu kutokana na matokeo tuliyopata na kinachoendelea, lakini kwa kweli siwezi kusubiri mchezo huo. Nina hamu kubwa ya kucheza,” amesema Carrick.
Ameongeza kuwa hawezi kutabiri kitakachotokea baadaye, lakini anataka mchezo huo uwe usiku mkubwa kwa Manchester United.
Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika Carrington, mshambuliaji Bryan Mbeumo na kiungo Carlos Baleba walionekana kuwa na ari kubwa, huku beki wa Argentina, Lisandro Martinez, naye akishiriki kikamilifu licha ya kupata kadi nyekundu dhidi ya Chelsea.
Kuhusu uwezekano wa kumuweka benchi Martinez kutokana na tukio hilo, Carrick amesema makosa ni sehemu ya mchezo wa soka na kila mchezaji anaweza kufanya maamuzi yanayoweza kuleta matokeo tofauti.
Pia amesisitiza kuwa hana mashaka na kujituma kwa Martinez wala wachezaji wengine wa kikosi chake.
“Ninachokiona ni kwamba chumba cha kubadilishia nguo kina hali nzuri. Sijawahi kutilia shaka kujituma kwa wachezaji kwa ajili ya klabu, mimi na wao wenyewe. Tunahitaji kucheza vizuri zaidi na kufanya maamuzi bora, lakini kujituma si tatizo,” amesema.
Kwa upande wake, kiungo wa England, Kobbie Mainoo, amesema kikosi hicho bado kina mshikamano na kina uwezo wa kubadilisha hali ya matokeo kwa kupata ushindi mmoja.
Mainoo, mwenye umri wa miaka 21, alirejea uwanjani dhidi ya Chelsea akiwa mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili baada ya kukosa mechi nne kutokana na majeraha ya misuli.
Amesema amekuwa Manchester United kwa muda mrefu tangu alipojiunga na akademi ya klabu hiyo akiwa na umri wa miaka saba, hivyo anaelewa changamoto na matarajio yanayoambatana na kuichezea timu hiyo.
“Manchester United ni klabu kubwa na nimejifunza kuwa kutakuwa na nyakati nzuri na mbaya. Hakuna safari inayokuwa rahisi wakati wote. Huu umekuwa msimu mgumu, lakini nahisi ushindi mmoja tu unaweza kubadilisha hali tuliyonayo,” amesema Mainoo.
Ameongeza kuwa nafasi ya sasa ya Manchester United haikubaliki kwa klabu yenye historia na ukubwa wake, akisisitiza kuwa ana wajibu wa kuendeleza misingi na utamaduni wa klabu hiyo alioujifunza tangu akiwa akademini.