Wachezaji wanaoshiriki Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) wanatarajiwa kunufaika na uwekezaji wa mwaka mmoja wenye thamani ya Sh588.9 milioni katika msimu wa 2026.
Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa juzi kati ya kampuni ya michezo ya kubashiri ya betPawa kwa ajili ya kuongeza udhamini kwa msimu mmoja, wachezaji watalipwa fedha hiyo kupitia mpango wa Locker Room Bonus (LRB) unaolenga kuwazawadia timu zinazoshinda.
Kupitia makubaliano hayo mapya, kila mchezaji wa timu itakayoshinda mechi atapokea Sh88,750 papo hapo, huku bonasi hiyo inawanufaisha makocha na maofisa wengine wa benchi la ufundi la timu husika baada ya kila ushindi.
Jumla ya wachezaji 12 pamoja na maofisa wanne wa benchi la ufundi, wakiwamo makocha wawili wa kila timu inayoshinda watanufaika na malipo hayo, hatua ambayo imelenga kuongeza thamani ya ushindi na kuhamasisha ushindani mkubwa katika ligi msimu mzima.
Meneja wa Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika wa betPawa, Bwalya Noah, alisema kampuni hiyo inaamini maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu yanaanza kwa kuwekeza kwa wachezaji.
“betPawa tunaamini mafanikio yanayopatikana uwanjani yanapaswa kuwanufaisha wale wanaoyaleta. Ndiyo msingi uliozaa mpango wa LRB. Timu inaposhinda, wachezaji na benchi la ufundi waliofanikisha ushindi huo wanapaswa kupata zawadi yao mara moja,” alisema Noah.
Alisema mpango huo unatambua juhudi za wachezaji, unazawadia ubora na kuhakikisha mafanikio ya uwanjani yanageuka kuwa manufaa ya moja kwa moja kwa wahusika.
Noah alisema LRB imekua na kuwa moja ya programu kubwa za maendeleo ya michezo barani Afrika, ikinufaisha maelfu ya wanamichezo katika nchi mbalimbali zikiwamo Ghana, Uganda, Nigeria na Cameroon, huku mamia ya wachezaji wa mpira wa kikapu nchini Tanzania tayari wakinufaika na bonasi hizo.
Kwa upande wake, mratibu wa Masoko wa betPawa Afrika Mashariki, Nassoro Mungaya, alisema kampuni hiyo inatarajia ushirikiano huo kuendelea kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu nchini.