Makundi ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 yametangazwa rasmi, huku baadhi ya klabu kubwa za Afrika Mashariki na Kati zikitarajiwa kukutana katika mechi zenye ushindani mkali.
Mabingwa wa Rwanda, APR FC, wamepangwa Kundi A pamoja na Vipers SC ya Uganda, Gor Mahia ya Kenya na Garde Républicaine ya Djibouti.
Kundi B linazikutanisha timu za Tanzania, Singida Black Stars na Simba SC, pamoja na Jamus SC ya Sudan Kusini na Mogadishu City Club ya Somalia.
Katika Kundi C, Al Hilal SC ya Sudan itamenyana na Rayon Sports ya Rwanda, Tusker FC ya Kenya na KVZ FC kutoka Zanzibar.
Michuano hiyo itafanyika nchini Rwanda na inatarajiwa kuvutia mashabiki wengi wa soka kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Waandalizi bado hawajatangaza ratiba kamili ya mechi, lakini upangaji wa makundi umeanza kuongeza hamasa kuelekea kuanza kwa mashindano hayo ya kila mwaka yanayoandaliwa na CECAFA.