Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, pamoja na benchi lake la ufundi, wamemtembelea kiungo wa Yanga SC, Pacome Zouzoua, hospitalini kwa ajili ya kumjulia hali baada ya kuumia katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pacome alipata majeraha hayo jana katika mchezo uliowakutanisha Yanga SC na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, baada ya kugongana na beki wa JKT Tanzania, Hassan Wahabi, na kulazimika kutolewa nje ya uwanja kwa matibabu.
Ziara ya Ibenge na benchi lake imepokelewa kama ishara ya mshikamano na utu katika mchezo wa soka, huku wakimtakia nyota huyo nafuu na kurejea haraka uwanjani.
Katika mchezo huo, Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26.
Baada ya mechi hiyo, JKT Tanzania ilitoa taarifa rasmi ikiomba radhi kwa Pacome na Yanga SC, ikieleza kuwa tukio lililosababisha majeraha hayo halikuwa la makusudi. Klabu hiyo pia ilimtakia mchezaji huyo uponaji wa haraka ili arejee kuendelea na majukumu yake uwanjani.
Hadi sasa, Yanga SC haijatoa taarifa rasmi kuhusu ukubwa wa jeraha la Pacome wala muda anaotarajiwa kukaa nje ya uwanja.