ATLANTA, Marekani: Nyota wa Hispania, Lamine Yamal, amesema bado hajawa 100% fiti na huenda asianze kikosi cha kwanza katika mechi yao ya pili ya Kombe la Dunia dhidi ya Saudi Arabia.
Yamal alifunguka kupitia kituo cha televisheni cha RTVE akieleza kuwa bado yupo katika mchakato wa kupona na kuzoea hali ya mashindano baada ya kuingia akiwa na jeraha la nyama ya paja la mguu wa kushoto.
“Niko sawa, nahisi vizuri, lakini bado mapema sana,” alisema Yamal. “Hakuna haja ya kuhatarisha. Nipo kwenye mchakato wa kuzoea hali, sio wakati wa kucheza mechi nzima bado. Lakini naweza kucheza dakika kadhaa kulingana na kocha.”
Katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Cape Verde, Yamal alicheza kama mchezaji wa akiba akitokea dakika ya 71, lakini hakuweza kusaidia Hispania kupata ushindi katika sare ya 0–0 dhidi ya timu hiyo iliyokuwa inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Hispania itaumana na Saudi Arabia siku ya Jumapili mjini Atlanta kabla ya kuelekea Guadalajara kumenyana na Uruguay katika mchezo mwingine muhimu wa Kundi H.
Yamal pia alisema mwenzake Nico Williams, ambaye naye aliingia na majeraha, yupo mbele zaidi yake katika kiwango cha utimamu wa mwili.
“Kimwili yeye yuko vizuri zaidi kuliko mimi,” alisema. “Hatujalazimisha chochote. Tuna timu nzuri yenye wachezaji wa kiwango cha juu na tunapaswa kwenda hatua kwa hatua.”
Licha ya umri wake mdogo, Yamal ameendelea kuwa miongoni mwa nyota wakubwa wa Hispania baada ya kung’ara na Barcelona na kusaidia Hispania kushinda Euro 2024. Umaarufu wake umeendelea kuongezeka nchini Marekani, ambapo picha zake zimeonekana kwenye matangazo makubwa karibu na uwanja wa Mercedes-Benz Stadium.
“Ninakubali kama kawaida, nimezoea,” alisema kuhusu umaarufu wake. “Najua ninachowakilisha ndani na nje ya Hispania. Ninajaribu kutoa bora yangu kila wakati.”