South Korea Yageuza Matokeo na Kuichapa Czech Republic 2-1 Kombe la Dunia 2026

GUADALAJARA, Mexico – Timu ya taifa ya Korea Kusini imeonyesha moyo mkubwa wa kupambana baada ya kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Czech Republic katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Dunia 2026 iliyochezwa Estadio Guadalajara.

Korea Kusini ilitawala sehemu kubwa ya mchezo kwa soka la pasi nyingi na mashambulizi ya kuvutia, huku nahodha Son Heung-min akiongoza safu ya ushambuliaji pamoja na Lee Kang-in na Lee Jae-sung.

Licha ya kutengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza, Korea Kusini ilishindwa kuzitumia na kujikuta ikiruhusu bao la kwanza dakika ya 59. Czech Republic walifunga kupitia Ladislav Krejci aliyepachika bao kwa kichwa baada ya kutokea kwa mpira mrefu wa kurushwa na Vladimir Coufal.

Bao hilo halikuwavunja moyo Wakor ea Kusini ambao waliendelea kushambulia kwa kasi wakisukumwa na mashabiki wengi waliokuwa uwanjani. Dakika nane baadaye, Hwang In-beom aliisawazishia timu yake baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Lee Kang-in kabla ya kuwapita walinzi wawili na kumalizia kwa ustadi mkubwa.

Korea Kusini waliendelea kutawala mchezo na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 80 wakati Hwang In-beom alipotoa pasi ya chini iliyomaliziwa nyavuni na mchezaji wa akiba Oh Hyeon-gyu na kuifanya timu yake kuongoza 2-1.

Czech Republic walijaribu kusaka bao la kusawazisha katika dakika za mwisho kupitia mipira ya adhabu na kurusha mipira mirefu, lakini walishindwa kuivunja safu ya ulinzi ya Korea Kusini.

Ushindi huo unaifanya Korea Kusini kuungana na Mexico kileleni mwa Kundi A baada ya wenyeji hao kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Korea Kusini Hong Myung-bo aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha nidhamu na kupambana hadi mwisho.

“Kabla ya mechi niliwaambia wachezaji mambo mawili; wasikate tamaa hadi mwisho na wacheze kama timu moja. Wamefanya hivyo kikamilifu,” alisema kocha huyo.

Matokeo hayo yanatoa ishara kwamba Korea Kusini inaweza kuwa moja ya timu zitakazotoa ushindani mkubwa katika michuano ya Kombe la Dunia 2026.