Rais wa sasa wa klabu ya Real Madrid, Florentino Pérez, anatarajiwa kushinda uchaguzi wa urais wa klabu hiyo kwa kupata takribani asilimia 65 ya kura, kwa mujibu wa exit polls zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya michezo vya Hispania.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kura zilizopigwa kwa njia ya posta bado hazijajumuishwa kwenye matokeo hayo ya awali, huku vyanzo vikieleza kuwa Pérez anaweza kuongeza zaidi tofauti ya kura hizo.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa usiku wa leo majira ya saa 10 kwa saa za Hispania.
Katika taarifa iliyotolewa mapema leo na Real Madrid, Bodi ya Uchaguzi ya klabu hiyo ilieleza kuwa hadi saa 11 jioni kwa saa za Hispania, jumla ya wanachama 23,593 walikuwa wamepiga kura katika uchaguzi wa Rais na Bodi ya Wakurugenzi.
Klabu hiyo ilisema idadi hiyo inawakilisha ushiriki wa asilimia 31.37 ya wapiga kura, huku vituo vya kupigia kura vikiendelea kubaki wazi hadi saa 2 usiku.