Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda amesema ziara ya mwana Soka Rio Frerdnand, italeta fursa kwa vijana wenye ndoto ya kukua kwenye mpira wa miguu kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.
Makonda amesema hayo leo, Mei 22, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ujio wa nyota wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya Taifa ya Uingereza, Reo Ferdinand.
Amesema ndoto yake kubwa ni kuona wachezaji wakubwa wakichukua vijana na kuwapeleka Ulaya kuwaendeleza ambapo alianza na Drogba na kufuatiwa na Rio ambaye ana mtandao mkubwa wa watu wa karibu wenye utaalamu wa michezo na biashara.
” Ndoto yangu kubwa ilikuwa Reo aje nchini kusaka vipaji vya watoto na awachukue, leo hii atatuma timu yake ya wataalamu kwenda Qatar kuangalia vijana wetu wa chini wa Umri wa miaka 17, ambao wanashiriki Kombe la Dunia, watakaofanya vizuri atawachukua” alisema Waziri Makonda
Naye Rio Ferdinand amesisitiza azma yake ya kuwainua watoto wa Kitanzania wenye vipaji vya soka kupitia taasisi yake iliyopo nchini Uingereza, ambayo inalenga kuwapa vijana fursa ya kukuza vipaji vyao kwa viwango vya kimataifa.