Nyota chipukizi wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Spain, Lamine Yamal, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kuonekana akiinua bendera ya Palestine wakati wa sherehe za ubingwa wa La Liga zilizofanyika mitaani Jumatatu.
Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya Barcelona kuifunga Real Madrid mabao 2-0 katika mchezo wa El Clásico, ushindi uliowahakikishia kutwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya 29 katika historia ya klabu hiyo.
Yamal, ambaye ameendelea kung’ara msimu huu akiwa mmoja wa nyota muhimu wa Barcelona licha ya umri mdogo, alionekana akiwa pamoja na mashabiki wakati wa sherehe hizo huku akibeba bendera ya Palestina, jambo lililoibua hisia tofauti kutoka kwa mashabiki wa soka na watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani.
Baadhi ya watu walitafsiri hatua hiyo kama ishara ya mshikamano na Palestina, huku wengine wakieleza kuwa kitendo hicho kinaonyesha namna wanasoka wakubwa wanavyoendelea kutumia umaarufu wao kuonyesha misimamo yao kuhusu masuala ya kimataifa.
Spain ni miongoni mwa mataifa ya Ulaya yaliyoonyesha msimamo wa wazi kuhusu kuitambua Palestina kama taifa huru, jambo ambalo limekuwa mjadala mkubwa katika siasa za kimataifa kwa miaka ya karibuni.