Maslahi ya kumtaka mshambuliaji wa Manchester United, Jadon Sancho, yanaendelea kuongezeka huku klabu mbalimbali zikianza kuonyesha nia ya kumsajili kuelekea dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa ripoti za Sky Sports, klabu moja kutoka Italia ambayo haijatajwa jina tayari imefanya mawasiliano ya awali kuulizia uwezekano wa kumsajili nyota huyo.
Wakati huohuo, Borussia Dortmund nao wamethibitisha kuanza mazungumzo ya kumrejesha Sancho, ambaye aliwahi kung’ara akiwa na klabu hiyo kabla ya kujiunga na United.
Mkataba wa Sancho ndani ya United unatarajiwa kumalizika msimu huu wa kiangazi, na tayari wawakilishi wake wanaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu zilizo nje ya England. Inaelezwa pia kuwa United hawana mpango wa kutumia kipengele cha kuongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi.
Kwa sasa, Sancho yupo kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa, na hana haraka ya kufanya maamuzi kuhusu hatma yake. Inaripotiwa kuwa anataka kuchambua chaguo zote alizonazo, huku uwezekano wa kubaki kwenye Premier League ukiwa bado upo wazi.