Sakata la mashabiki kufanya vurugu, Yanga SC yatuma ujumbe kwa timu zote

Ali Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga SC amesema kuwa ni muhimu kwa mashabiki wa timu zote kuacha kufanya vurugu uwanjani kwa kuwa adhabu ambazo zinatolewa ni kubwa na hasara kwa timu.

Machi 19,2026 tarifa kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) ilieleza  Yanga SC imetozwa faini ya milioni 5 kwa kosa la mashabiki kurusha chupa za maji kwa waamuzi mechi namba 104, Azam FC 0-0 Yanga SC.

Kamwe amesema: “Napenda kuwaomba wanachama na mashabiki wote kudumisha ustaarabu wanapofika uwanjani. Ujumbe huu wa wanachama na mashabiki kurusha chupa na kufanya vurugu uwanjani nauwasilisha si kwa Yanga SC tu bali kwa niaba ya vilabu vyote kwa kuwa nina dhamana ya Uenyekiti wa Vilabu.

“Hii ni mara ya pili kwa klabu yetu kutozwa faini ya aina hii. Ni muhimu kufahamu kuwa adhabu hizi zina athari kubwa kifedha na zikiendelea mwisho wake hautakuwa mzuri kwa maendeleo ya klabu yetu.

“Ni kweli kwamba ligi yetu kwa sasa imechangamka na ina ushindani mkubwa lakini iwapo hali hii itaendelea madhara yake yatakuwa makubwa kwa maendeleo na heshima ya soka letu,”.

 Pia mchezo wa ligi namba 72, Singida Black Stars FC 0-3 Yanga SC, wametozwa milioni 5 na kutakiwa kulipa gharama za matengenezo ya madirisha na maeneo mengine ya chumba cha kuvalia yaliyoharibiwa na mashabiki wake.

***

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo na Moyo Wangu Unavuja Damu.  Kuvipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371.

Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Msichana wa Maisha Yangu, jiandae kuipata.