KOCHA Mkuu wa Yanga, raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, amesema kuwa ujio wa kiungo mshambuliaji, Mkongomani, Chico Ushindi, umeongeza ubora na ushindani wa namba katika kikosi chake.
Kauli hiyo aliitoa siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania uliotarajiwa kupigwa jana saa kumi kamili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Kabla ya mchezo huo, kocha huyo alitangaza kuwepo hatihati ya kumtumia kiungo wake mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutokana na majeraha.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nabi alisema kuwa licha ya kuwepo hatihati ya kumtumia Fei Toto, lakini yupo Chico ambaye anamudu kucheza nafasi hiyo namba kumi.
Nabi alisema kuwa anaamini uwezo mkubwa alionao Chico kutokana na kumfahamu baada ya kumfuatilia tangu akiwa klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.
Aliongeza kuwa Chico ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja namba 7, 10 na 11 hivyo uwepo wake katika timu, unampa nafasi kubwa ya kuwepo katika kikosi chake cha kwanza.
“Chico ana faida kubwa katika timu, hiyo ni kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja katika timu, hivyo ninaamini atatoa mchango mkubwa katika timu.
“Katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, huenda tukamkosa Fei Toto kutokana na majeraha, lakini tayari yupo Chico mwenye uwezo wa kucheza nafasi yake.
“Hivyo ushindani utaongezeka katika timu baada ya Chico kuja, hivi sasa kilichobakia kwake ni kuingia katika mfumo ambacho ni kitu kidogo, hilo ni jukumu langu ambalo nitalifanya,” alisema Nabi.