VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamerejea salama Dar baada ya kutoka kusaka pointi sita ugenini.
Walianza mbele ya Coastal Union mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga na ubao ukasoma Coastal Union 0-2 Yanga.
Mabao ya Fiston Mayele na Said Ntibanzokiza yalitosha kuipa pointi tatu mazima Yanga.
Kituo kilichofuata ilikuwa mbele ya Polisi Tanzania, Januari 23,Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na ubao ulisoma Polisi Tanzania 0-1 Yanga.
Ni pointi 35 zilizopo kwenye akaunti ya Yanga huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja mpaka muda huu katika mzunguko wa kwanza.
Polisi Tanzania inayonolewa na Kocha Mkuu, Malale Hamsini ipo nafasi ya tano na pointi zake ni 18 kibindoni.
Bao la Dickson Ambundo lilitosha kuipa ushindi Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Ambundo amesema kuwa ni furaha kwake kufunga kwa ajili ya timu pamoja na mashabiki jambo ambalo kila mmoja anapenda.
“Napenda kwa kuwa nimefunga kwa ajili ya timu, wakati huu ni furaha kwetu na mashabiki, nilikuwa kwenye majeruhi lakini nimerudi hilo ni jambo la kumshukuru Mungu,”.